Pogba, De Gea kuikosa Manchester United, Liverpool

Muktasari:

Kipa namba mbili Sergio Romero anategemewa kucheza mechi yake ya kwanza ya ligi baada ya miezi 17, wakati Man United ikivaa Liverpool timu inayokaribia rekodi ya Manchester City ya kushinda mechi 18 mfululizo za Ligi Kuu England.

London, England. Manchester United itawakosa nyota wake David de Gea na Paul Pogba katika mchezo wao muhimu dhidi ya Liverpool utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja Old Trafford.

De Gea ameongeza orodha ya majeruhi United baada ya kuumia nyonga wakati akichezea Hispania katika mchezo wa kufuzu kwa Euro 2020 dhidi ya Sweden.

Kipa huyo anatakiwa kufanyiwa vipimo na madaktari wa timu yake wakati atakaporejea Carrington leo Alhamisi, lakini kocha Ole Gunnar Solskjaer amekiri jana usiku kuwa haoni kama ataweza kucheza mechi hiyo.

'David anahitaji kufanyiwa vipimo,' alisema bosi huyo wa United. 'Nafikiri atakuwa kwa muda. Ni mapema kutabiri atakuwa nje kwa muda gani.'

Kipa namba mbili Sergio Romero anategemewa kucheza mechi yake ya kwanza ya ligi baada ya miezi 17, wakati Man United ikivaa Liverpool timu inayokaribia rekodi ya Manchester City ya kushinda mechi 18 mfululizo za Ligi Kuu England.

Man United pia itamkosa kiungo wake Pogba ambaye bado anauguza majeraha ya kifundo cha mguu akiwa amecheza mechi mbili tu tangu Agosti.

Mfaransa huyo amereja Dubai katika hali ya hewa ya joto kuendelea na matibabu ya mguu huo yatakayomweka nje hadi mwisho wa mwezi huo.

Alipoulizwa kuhusu uwepo wa Pogba katika mchezo wa Liverpool, Solskjaer alisema: 'Hakuna nafasi kwake. Paul ameumia, kurudi itachukua muda kidogo kutokana na kusumbuliwa na maumivu.

Man United inatumaini nyota wake kadhaa waliokuwa majeruhi watarejea mapema kabla ya mchezo huo wa Jumapili, lakini Luke Shaw, Jesse Lingard na Diogo Dalot bado hali zao hazijatengema.

Anthony Martial, ambaye hajacheza kwa zaidi ya miezi miwili, yupo fiti lakini hajafanya mazoezi na wenzake ikiwa ni siku tatu kabla ya mechi ya Liverpool.

Aaron Wan-Bissaka naye yupo katika hali hiyo baada ya kukosa michezo mitatu iliyopita kutokana na kusumbuliwa na majeruhi.