Rais Magufuli atuma salamu kwa Taifa Stars

Tuesday June 25 2019

 

By Emmanuel Mtengwa, Mwananchi

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewataka wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars' kutokukata tamaa na waendelee kujituma katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019.

Pia, amewataka wananchi kuwaombea wachezaji wa Stars kwa kuwa kushindwa kwao ni kushindwa kwa Tanzania na kushinda kwao ni ushindi wa Watanzania

Rais Magufuli ametuma salamu hizo leo Jumanne Juni 25, 2019 akiwa kwenye uzinduzi wa ghala na Mitambo ya Taifa Gas uliofanyika Kigamboni.

“Nakuruhusu nenda, si umesema ukienda tutashinda, kapande ndege leo nenda na ukawaambie wachezaji wasikate tamaa, kwenye uwanja wa mpira kuna kushinda na kushindwa,” amesema Rais Magufuli wakati akimpa salamu za Stars Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

 

“Kwa hiyo wao wakazane, wakajitume zaidi na sisi tuendelea kuwaombea kwa sababu kushindwa kwao ni kushindwa kwetu Watanzania na kushinda kwao ni kushinda kwetu Watanzania” amesema

Advertisement

Awali, Makonda akitoa salamu za mkoa kwenye uzinduzi wa ghala hilo alimuomba Rais Magufuli ruhusa ili aende kushuhudia michuano hiyo inayofanyika nchini Misri.

“Rais najua wewe ni mpenzi wa mpira, neno lako la kuwatia moyo vijana hawa litaongeza hamasa kubwa sana na chachu” amesema Makonda na kuongeza

“Nilikuwa natamani tamani kuomba kibali angalau niende kule kambini (Misri), ikikupendeza nikashiriki nao.”

Taifa Stars inayoshiriki michuano ya Afcon 2019 imepoteza mechi ya kwanza kwa kufungwa mambao 2-0 na Senegal na inatarajia kushuka dimbani Alhamisi kucheza mechi ya pili dhidi ya na Timu ya Taifa ya Kenya “Harambe Stars”

Advertisement