Rais TFF aitibua Chadema kumtaja Lissu ‘kuikashifu Serikali’ , atakiwa kuomba radhi

Muktasari:

  • Kauli ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia  kumfananisha mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Michael Wambura kwa kupinga hoja, kumeiibua Chadema na kumtaka rais huyo kuomba radhi hadharani

Dar es Salaam. Kauli ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia  kumfananisha mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Michael Wambura kwa kupinga hoja, kumeiibua Chadema na kumtaka rais huyo kuomba radhi hadharani.

Chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimetaja mambo manne kinachoazimia kuyatekeleza iwapo Karia hatoomba radhi.

Leo Jumamosi Februari 2, 2019 jijini Arusha katika mkutano mkuu wa TFF Karia alikemea watu wenye tabia za ‘u Tundu Lissu’ katika soka, kwamba kamwe hawezi kukubali kuona wakiendelea kukosoa uongozi wa TFF.

Baada ya mkutano huo Karia alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu kauli hiyo amesema, “Nimesema kama kuna ‘ma Tundu Lissu’ kwenye mpira, nadhani mnaelewa Lissu anahangaika kwenye vyombo vya habari kuikashifu Serikali, na Wambura anazungumza kwenye vyombo vya habari kuikashifu TFF na uongozi wa TFF.”

“Hivyo nikamlinganisha Wambura na Lissu, ila kama hii kauli imewakera wengine naomba samahani.”

Kufuatia kauli hiyo, leo jioni mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alitoa tamko la chama hicho, akimtaka Karia kuomba radhi.

“Tumepokea kauli yenye ukakasi mkubwa (ya Karia) kuwa atawashughulikia wale wote ambao wataleta ‘ U-Tundu Lissu’ kwenye mpira. Kauli hii imebeba ujumbe mahsusi kuwa watu aina ya Tundu Lissu wanastahili kushughulikiwa kwenye sekta zote,“ amesema Mrema.

Amebainisha kuwa chama hicho kinaamini kuwa watu aina ya Lissu ni wale wote wenye mtazamo na uwezo wa kuhoji,  wanaotaka utawala wa sheria ufuatwe na wanaotaka sheria na Katiba ziheshimiwe.

“Sasa kauli ya Karia inatufanya tujiulize maswali inawezekana anawajua waliomshughulikia Lissu na ndio maana anataka kuwatumia kushughulikia 'Tundu Lissu' walioko kwenye mpira,” alisema Mrema.

Lissu alishambuliwa mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake Area D, mjini Dodoma wakati akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge. Alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Alipata matibabu katika hospitali hiyo hadi Januari 6, kwa sasa ameruhusiwa kutoka Hospitali lakini bado anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji.

Tangu Septemba 7, 2017 hadi Desemba 31, 2018, mwanasheria huyo mkuu wa Chadema ametibiwa kwa kipindi cha siku 480 sawa na mwaka mmoja, miezi mitatu na siku 24.      

Kuanzia Januari 14, 2019 Lissu ameanza ziara barani Ulaya akidai ataeleza kwa kina kile alichoandika katika waraka alioutoa kwa ajili ya mwaka 2019.

Ziara ya Lissu inaanza baada ya Desemba 31, 2018 kuhitimisha safari ya matibabu aliyoanza baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa zaidi ya risasi 30 mjini Dodoma muda mfupi baada ya kutoka kuhudhuria kikao cha mchana cha Bunge.

Katika mahojiano yake na Mwananchi Lissu amesema baada ya kutoka Uingereza ambako alifanya mahojiano na Shirika la Utangazi la BBC la nchini humo, amepata mwaliko mwingine wa kwenda katika ofisi za Umoja wa Ulaya (EU) zilizopo Brussels, Ubelgiji na baadaye ataelekea Marekani na katika ziara hizo amesema ataelezea kile kilichomtokea Septemba 7, 2017, hali ya kisiasa nchini na mambo mengine.

Katika maelezo ya leo ya Chadema, chama hicho kimesema kufuatia kauli hiyo ya Karia kinatafakari kufanya mambo manne ambayo ni; kuhamasisha wanachama wake kutoshiriki matukio ya TFF, kususia bidhaa zote zenye nembo na au zinazotolewa na TFF zikiwemo jezi za timu za Taifa, kuchukua hatua dhidi ya kampuni zitakazoendelea kushirikiana na TFF na kushawishi wadau wa mpira kutoshirikiana na TFF.