Ronaldo atwaa tuzo usiku wa Messi akinyakuwa Ballon d'Or

Muktasari:

Ronaldo ametwaa tuzo ya Mchezaji bora wa Mwaka wa Serie A katika usiku ambao Messi ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia

Milan, Italia. Cristiano Ronaldo ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Serie A katika usiku ambao mpinzani wake Lionel Messi ametwaa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa duniani Ballon d'Or.

Mshambuliaji huyo Mreno hakutokea katika sherehe za kutolewa kwa tuzo ya Ballon d'Or jijini Paris kwa sababu alikuwa akishinda tuzo yake nyingine jijini Milan.

Messi ametwaa Ballon d'Or kwa mara ya sita akimpiku Ronaldo aliyechukua tuzo hiyo mara tano.

Nyota huyo wa Barcelona alimpiku beki wa Liverpool, Virgil van Dijk ambaye amekuwa na bahati mbaya na tuzo hiyo pamoja na kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa,  Super Cup na tuzo ya mchezaji bora wa Mwaka wa UEFA.  

Messi mwenye miaka 32, alikuwa ametabiliwa ushindi na watabiri baada ya kuvuja kwa ripoti iliyoonyesha Messi ameshinda tuzo  hiyo saa moja kabla ya kufanyika kwa sherehe hiyo.

Watu walishangazwa mwaka jana wakati alipokuwa nafasi ya tano, lakini mafanikio yake msimu huu ndani ya Barcelona yamemfanya kuweka rekodi ya kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya sita.

Hii ni mara ya kwanza tangu 2015 kwa Messi kunyakuwa tuzo hiyo huku Ronaldo (akitwaa mara mbili) na nyota mwenzake wa zamani wa Real Madrid, Luka Modric akitwaa mara moja.