Rooney kupata dili Derby county

Friday October 16 2020
rooney pic

DERBY, ENGLAND. MCHEZAJI wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Derby County kama kocha mchezaji ana asilimia zaidi ya 70 kuwa kocha mpya wa klabu hiyo baada ya kocha wa sasa Phillip Cocu kuripotiwa kuwa kwenye kuti kavu na anaweza kufukuzwa muda wowote.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na tovuti ya The Sun, Cocu amekuwa kwenye presha kubwa baada ya Derby kuwa kwenye kiwango kibovu ikiwa imeshinda mechi moja katika mechi nne za ufunguzi wa Ligi Daraja la Kwanza nchini England na kuifanya ishike nafasi ya 20 katika msimamo.

County leo itakuwa inacheza dhidi ya Watford ambapo ikiwa itapoteza ndio unaweza ukawa mwisho wa kocha huyo kutoka Uholanzi baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Norwich ambao ulichezwa kabla ya kuanza kwa wiki ya michuano ya kimataifa.

Mmiliki wa klabu hiyo, Mel Morris anaamini ikiwa timu yake itapoteza mchezo wa Ijumaa itakuwa ni ishara mbaya na itafanya mashabiki wazidi kupiga kelele hivyo anafikiria kumpa mikoba Rooney ambaye ana matumaini anaweza kuikomboa timu hiyo kutoka shimoni.

Kocha wa zamani wa County, John Gregory atazamiwa kuwa msaidizi wa Rooney ikiwa atapewa mikoba kwa sababu hana uzoefu wa kutosha hivyo atakuwa msaada wa kumuelekeza Rooney nini kifanyike.

Advertisement