Sadio Mane amjibu Pep kujirusha kama kawa

Friday November 8 2019

 

LIVERPOOL, ENGLAND . STAA Sadio Mane amesema ataendelea kujiangusha kupata penalti kwa ajili ya kuisaidia Liverpool.

Fowadi huyo wa kimataifa wa Senegal alishutumiwa na Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola kuwa amekuwa akijiangusha ili kupata penalti, wakati alipofanya hivyo kwenye mchezo dhidi ya Aston Villa wikiendi iliyopita.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alimjibu Guardiola akisema Mane hajiangushi, lakini mchezaji mwenyewe amesema hatabadilisha staili yake ya kiuchezaji Jumapili wakati watakapokabiliana na Man City kwenye Ligi Kuu England.

Mane alisema: “Kama nikiona itakuwa penalti bila ya shaka nitajiangusha. Kama kufanya hivyo ni penalti, nitafanya, kwanini nisifanye?”

Mane alionyeshwa kadi ya njano kutokana na kujiangusha na kujitetea akiungana na kocha wake: “Lakini anachokisema Jurgen ni sahihi. Mimi sijiangushi.”

Mane anaamini maneno hayo ya Guardiola yanaweza kumshawishi Mwamuzi Michael Oliver kumtolea macho zaidi kwenye mchezo wa timu zao utakaofanyika Anfield.

Advertisement

Jumapili hii, Liverpool itakuwa mwenyeji wa Manchester City pale Anfiled.

Advertisement