Samatta apewa unahodha Genk ikishinda 3-1 nyumbani

Sunday September 22 2019

 

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa timu ya Taifa Tanzania, Mbwana Samatta akiwa nahodha kwa mara ya kwanza ameiongoza Genk kupata ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya KV Oostende kwenye Uwanja wa Luminus Arena.

Katika mchezo huu Samatta alipewa kitambaa cha unahodha akiwaongoza wenzake kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika uwanja wao wa nyumbani.

Genk ilikuwa wa kwanza kupata goli dakika 18 kwa Ronald Vargas aliyejifunga, lakini Oostende walirudisha dakika 32 kupitia kwa Idrissa Sylla.

Baada ya goli hilo Oostende walionekana kuamka na kutafuta goli la kuongoza, lakini walikuwa wanakutana na changamoto ya kupenya safu ya ulinzi ya Genk.

Dakika 44 mshambuliaji Paul Onuachu aliifungia goli Genk na kuinua shangwe kwa mashabiki waliokuwa kwenye uwanja wa Luminus Arena.

Goli hilo liliwapa nguvu mashabiki na wachezaji wa Genk kuzidi kupambana mpaka dakika 90, Sander Berge kufunga bao la tatu na kuwatuliza kabisa wapinzani wao.

Advertisement

Samatta kwenye mchezo huu alicheza dakika zote 90 huku akionekana kuwa nahodha mzuri baada ya kuwaelekeza wenzake pale wanapokuwa wamekosea.

Advertisement