Sevilla wakaribishwa na ngoma za asili

Muktasari:

  • Sevilla ni timu ya pili kubwa kutoka Barani Ulaya kutua nchini chini ya udhamini wa Sportpesa ambapo timu ya kwanza kufanya hivyo ilikuwa ni Everton iliyokuja mwaka 2017

Dar es Salaam. Burudani ya ngoma za asili inaendelea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam ikipamba mapokezi ya timu ya Sevilla kutoka Hispania.

Msafara wa timu hiyo umewasili mnamo saa mbili kasoro usiku ukiwa na takribani watu 62 kwa ajili ya mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Simba keshokutwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Kikundi hicho cha ngoma kinachotoa burudani uwanjani hapo kinaongozwa na mwanamuziki aliyejizolea sifa kwa kutunga mashairi, Mrisho Mpoto na kilianza kutumbuiza tangu nyakati za saa 1 usiku.

Msafara wa Sevilla umepokewa na wadau mbalimbali wakiongozwa na Mkurugenzi wa Utawala wa Kampuni ya ubashiri wa matokeo ya SportPesa, Tarimba Abbas.

Upande wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), aliyekuwepo kwenye mapokezi ya Sevilla ni mwenyekiti wa kamati ya mashindano, Alhaji Msafiri Ahmed Mgoyi aliyemuwakilisha Rais wake Wallace Karia aliyeambatana na Ofisa Protokali, Rafael Matola.

Luis Cardenas ambaye ni mwakilishi wa Ligi Kuu ya Hispania nchini, naye alikuwemo kwenye mapokezi hayo lakini pia maofisa kadhaa wa Bodi ya Utalii na Wizara ya Maliasili na Utalii nao walihudhuria