Shaibu ‘Ninja’ ashangaa uchezaji wa Yanga, KMC

Muktasari:

Beki wa zamani wa Yanga ameishauri timu hiyo kusajili dirisha dogo ili kuboresha safu ya ushambuliaji na winga ambao watakuwa chachu ya kufunga mabao mengi.

Dar es Salaam. Beki wa LA Galaxy ya Marekani, Abdallah Shaibu 'Ninja' alikuwepo jukwaani akishuhudia Yanga ikilazimishwa sare 1-1 na KMC ameshangazwa timu yake ya zamani kucheza soka la kupooza.

Ninja aliyeichezea Yanga kabla ya kujiunga na LA Galaxy mwanzoni mwa msimu amerejea nchini katika mapumziko wakati huu wakati Ligi ya Marekani imesimama kupisha majira ya baridi.

Akizungumzia mechi ya jana kati ya Yanga na KMC, Ninja alisema katika mchezo huo ameona walikuwa wanacheza kwa kupooza kama vile wachezaji wamechoka, kitu ambacho si kizuri kwa Yanga inayohitaji ubingwa.

"Si Yanga wala KCM, walicheza kwa kupooza sana, imeonekana kama wachezaji wamechoka pengine ratiba ya ligi inawabana, ila wanahitaji kujitofautisha na timu nyingine ili kuchukua ubingwa,"

"Wachezaji wazawa wajaribu kuwapa nafasi, kwani wanakuwa wanajua ligi ilivyo kuliko wageni ambao nimeona wanakwama kidogo," alisema Ninja.

Jambo lingine ambalo alikuwa makini sana kulifafanua kwamba hataki kuingilia majukumu ya benchi la ufundi ila alishauri wachezaji wangecheza kwenye namba zao kama Jafary Mohamed.

"Mohamed jana alicheza kiungo, naonag anakuwa mzuri zaidi akicheza kama beki, Papy Tshishimbi na kina Daud Raphael ama Makapu ndio wangecheza kiungo ndio maana nasema sitaki kuingia sana huko," alisema Ninja.