Simba Queens kupaa Ujerumani

Muktasari:

Kikosi cha timu ya wanawake ya Simba Qeeens, kinatarajia kuanza safari Jumapili hii kwenda Ujerumani kwa ajili ya kambi na kuwatafutia wachezaji wao nafasi ya kucheza nje.

TIMU ya soka ya Wanawake ya Simba Queens itakwea pipa kwenda Ujerumani Jumapili hii na kesho Alhamisi watakuwa Ofisi za Wizara ya Michezo kwa ajili ya kukabidhiwa Bendera ya Tanzania.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori amesema, timu yao itakwenda huko kutokana na ushirikiano na Taasisi ya St.Thomas na dhumuni lao ni kuona baadhi ya wachezaji wanapata nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa.
Magori alisema, wataondoka wachezaji 15, wataalamu wa benchi la ufundi wanne kwa nguvu ya
St Thomas na uongozi wa Simba utamgharamia mkuu wa msafara ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Asha Baraka.
"Timu itakaa Ujerumani kwa muda wa wiki mbili na itacheza mechi tifauti na baadhi ya timu kubwa za kike na zile ambazo zinahitaji wachezaji wenye vipaji, tumaimani kubwa safari hiyo itazaa matunda kwa baadhi ya wachezaji wetu ambao watakwenda huko watapata nafasi ya kucheza soka nchini humo,"
alisema Magori.
"Ni mwanzo mzuri kwetu, timu ya Simba Queens ya sasa imeanza kuwa na mipango  thabiti ya kuhakikisha inakuwa imara na uwezo wa kuchukua makombe mwakani na misimu mingine kama ilivyokuwa ya wanaume.
"Tunaendelea kufanya usajili wa wachezaji wazuri ambao tutawapa ada ya usajili lakini timu yetu ni miongoni mwa chache zinazolipa mishahara ingawa haifanani kwa ukubwa na ile ya wanaume lakini  wanapata."