Simba inaendeshwa kwa hasara-Mo Dewji

Muktasari:

Pamoja na hasara ambayo Simba imepata ndani ya kipindi hicho, Dewji ametamba kuwa utekelezaji wa mipango ya muda mrefu, kati na mfupi iliyowekwa na klabu utafanyika kama ilivyopangwa.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji amefichua kuwa klabu hiyo kwa sasa inaendeshwa kwa hasara, japo mikakati ya baadaye ni kuhakikisha inazalisha faida.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu masuala mbalimbali ya ndani ya klabu hiyo, Dewji alisema gharama za uendeshaji wa Simba zinazidi mapato wanayovuna.

Dewji, ambaye alikuwa akizungumza kwa mara ya kwanza tangu kufanya uwekezaji mkubwa ndani ya Simba, alisema: “Tangu tulipofanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu mpaka sasa ni hasara na hili katika biashara ni jambo la kawaida ingawa tunajua faida itakuja baadaye.

“Hata faida ikianza kupatikana, kinachofuata ni kuendelea kuwekeza fedha kwenye klabu kwa kuwa lengo si kutengeneza fedha bali kuifanya klabu iwe na msingi endelevu wa kujiendesha. Hata mimi au Swedi Nkwabi (Mwenyekiti wa Simba) tukija kuondoka, Simba iweze kujisimamia.” Hata hivyo, Dewji hakuweka wazi hasara ambayo Simba inaingia kwa sasa ikiwa ni miezi tisa tu tangu wanachama walipopitisha rasmi mabadiliko ya katiba ya klabu hiyo na kuruhusu mfumo wa uwekezaji.

Mabadiliko hayo yalipitishwa rasmi Mei mwaka jana ambapo pamoja na mambo mengine, Dewji alitangazwa kuwa mwekezaji mkuu ndani ya klabu hiyo.

Pamoja na hasara ambayo Simba imepata ndani ya kipindi hicho, Dewji ametamba kuwa utekelezaji wa mipango ya muda mrefu, kati na mfupi iliyowekwa na klabu utafanyika kama ilivyopangwa.

Mipango hiyo ni ujenzi wa uwanja na miundombinu ya klabu, usajili wa wachezaji wenye viwango bora, uboreshwaji wa idara mbalimbali ndani ya klabu na kuimarisha benchi la ufundi.

“Kusajili kampuni ya Simba tumemaliza, zoezi linalofuata ni kutangaza ajira katika idara zote, hivyo mwenye sifa ataomba na kufanyiwa usaili kwa vigezo vitakavyowekwa. Kwenye hili tutakuwa makini ili kupata watu sahihi kwani hii ni kazi na ni kampuni.

“Kuhusu ujenzi wa uwanja wetu, kuna vitu vya kiserikali vimekwamisha ila hatua zote za awali zipo tayari, tunasubiri serikali tu ili tumalizie,” alisisitiza Dewji.

Alisema ujenzi wa uwanja ni miongoni mwa malengo ya kati na watahakikisha unakuwa na kituo cha kisasa ikiwamo hosteli kwa ajili ya wachezaji ili kuifanya klabu kuwa na hadhi ya kimataifa.

Kuhusu ushiriki wa Simba kwenye mashindano ya kimataifa, Dewji alikiri kwa sasa bado hawana msuli wa kupambana na timu zilizopiga hatua kubwa kisoka, lakini anaamini muda mfupi ujao watafanya vizuri kulingana na malengo waliyojiwekea.

“Kwanza wote tuliumia kufungwa mara mbili mfululizo, lakini ni mambo yanayotokea kwenye mpira na ili ufanye makubwa ni lazima uwe na bajeti kubwa na maandalizi ya muda mrefu.

“Tunakoelekea ni kupandisha bajeti ili tufikie malengo yetu ya muda mrefu ambayo ni kutwaa ubingwa wa Afrika. Huwezi kuwa na bajeti kama ya sasa halafu ufikie malengo ya muda mrefu wakati wenzetu wanasajili wachezaji kwa mabilioni. Na sisi tutalazimika kununua wachezaji wa aina hiyo,” alisema Dewji.

Katika mkakati huo, Dewji alisema Simba itawashughulikia wachezaji wote wasio na nidhamu na wale wasiojituma na kusajili wale ambao watajitolea na kupigania nembo ya klabu.

Katika hatua nyingine, Dewji pia alitangaza mkakati wa klabu hiyo kuhakikisha wanafanya vizuri mechi zilizosalia za hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika hasa mchezo wa Jumanne ijayo na Al Ahly ya Misri. Katika kuhakikisha Simba inashinda mchezo huo, Mo alitangaza kuwa kiingilio kwa eneo la mzunguko kitakuwa Sh 2,000 tu ili kupata kundi kubwa la mashabiki kuipa sapoti timu yao