Simba yaanza na wakali watatu, Mwamnyeto uhakika

Mwananchi Digital imejiridhisha kwamba suala la beki wa kati Bakari Nondo Mwamnyeto kuvaa uzi wa Simba msimu ujao ni uhakika.

Lakini ndani ya wikiendi hii mchakato wa kuwaongeza mikataba wachezaji wao wanaowahitaji utakamilika kwa asilimia kubwa kwani Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Bilionea kijana Mohammed ‘Mo’ Dewji ametaka ishu hiyo imalizike mapema.

Taarifa za uhakika ambazo Mwananchi inazo ni kwamba wachezaji watatu wa kikosi hicho cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga na Shiza Kichuya ndio walioanza nao.

Kichuya ambaye hajawa na msimu mzuri alikuwa na mkataba wa miezi sita wa mkopo kutokea Misri.

Mzamiru tayari ameshasaini mkataba mpya wa miaka miwili ambao utamalizika msimu 2021-22, wakati Dilunga anasubiri kuwekewa pesa katika akaunti yake na kurekebishiwa kipengele cha kuongezewa mshahara kuwa mkubwa zaidi ya ule wa awali kama ambavyo amehitaji ili kumwaga wino.

Habari zinasema Kichuya amechukizwa na suala la kuwekwa benchi mara kwa mara na kocha Sven Vandenbroeck, lakini viongozi wakamwambia hiyo ni ishu ndogo ila na yeye aongeze juhudi ndio akakubali kuongeza mkataba na muda wowote baada ya kuingiziwa mkwanja wake katika akaunti atasaini dili jipya wikiendi hii.

Kichuya tangu ametua Simba katika dirisha dogo ameichezea timu hiyo mechi mbili tu, dhidi ya JKT Tanzania ambayo ilikuwa ya ligi aliyotumika kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza tu na mchezo mwingine ulikuwa wa Kombe la Shirikisho (FA), dhidi ya Stand United aliocheza kwa dakika 62.

“Baada ya hapo nadhani tutahamia kwa kiungo mwingine Said Ndemla ambaye naye pia mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu,” alisema mmoja wa viongozi mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba.

Mzamiru alipoulizwa alisema; “Kuhusu masuala ya kusaini mkataba mpya Simba nadhani hilo watalizungumzia uongozi kwani mkataba wangu unaelekea ukingoni lakini bado hata msimu wa kimashindano pia bado haujaisha.

“Nahitaji utulivu wa hali ya juu kwangu kufikiria zaidi kucheza katika kiwango cha hali ya juu ili kutoa mchango wangu katika timu ili kuchukua ubingwa wa ligi na FA,” alisema Mzamiru.

MSIKIE SENZO

Uongozi wa Simba kupitia kwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa alisema katika kikosi chao kabla ya kuanza kuwasajili wachezaji wapya watawabakisha wale wote ambao mikataba yao inamalizika kama benchi la ufundi likiwahitaji.

Alisema; “Tunabajeti ya kutosha kukamilisha dili za wachezaji hao muhimu wote ambao mwisho wa msimu huu wanamaliza mikataba. Halitakuwa jambo la kupendeza mnasajili wachezaji wapya wakati tuliokuwa nao ndani wanamaliza mikataba yao halafu tutashindwa kuongea nao lolote. Itakuwa si heshima kwa upande wao, ndio maana tunataka kuweka nguvu kubwa kwa ambao tunao na baada ya hapo mipango mingine itafuata.”

Wengine ambao mikataba inamalizika ni Yusuph Mlipili, Pascal Wawa, Shiza Kichuya na Sharaf Shiboub.