Simbu apania makubwa New York Marathoni

Tuesday October 16 2018Mwanariadha Alphonce Simbu

Mwanariadha Alphonce Simbu 

By Imani Makongoro, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mwanariadha Alphonce Simbu amesema anataka kuweka rekodi mpya ya muda, katika mbio za New York Marathoni zitakazofanyika Novemba 4, Marekani.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Simbu alisema pia anataka Sh200 milioni anazopata bingwa wa mbio hizo zinazokutanisha wanariadha nyota duniani.

Nyota huyo anayetarajiwa kuondoka nchini Oktoba 30, anawania dola 100,000 na bonasi dola 10,000 kwa mwanariadha atakayemaliza mbio saa 2:10:00 wanaume na saa 2:05:30 atapata bonasi ya dola 50,000 .

Bingwa mtetezi anayetoka Kenya, Geoffrey Kamworor, mshindi mara tano wa Olimpiki, Bernard Lagat, Wilson Kipsang, Lelisa Desisa, Tamirat Tola, Daniel Wanjiru (bingwa wa London marathoni 2017), mshindi mara nne wa Olimpiki raia wa Marekani, Abdi, Shadrack Biwott, Chris Derrick, Scott Fauble, Tim Ritchie na Scott Smith ni miongoni mwa nyota wanaotarajiwa kutoa upinzani kwa Simbu katika mbio hizo.

"Sina hofu ya ushindani wote tumejiandaa tutapambana siku ya mbio. Mbio ni ngumu, lakini ushindi ni malengo na kujipanga, niko fiti, nimejiandaa na ninachokifikiria siyo fedha ya zawadi pekee, pia kuweka rekodi ya muda mzuri," alisema Simbu.

Mshindi huyo wa medali ya shaba ya dunia ya marathoni, ana rekodi ya kukimbia kwa saa 2:09 na Kamworor alitumia saa 2:10 kushinda New York City Marathoni mwaka jana.

Advertisement

Simbu ambaye ni bingwa wa Mumbai Marathoni mwaka juzi, yuko kwenye orodha ya wanariadha watano bora wa Olimpiki katika mbio za marathoni baada ya kumaliza katika nafasi ya tano kwenye Olimpiki ya Rio 2016, Brazil.

Mwaka jana pia alitwaa medali ya dunia ya shaba kwenye marathoni katika mashindano yaliyofanyika Uingereza na mwaka huo alimaliza katika nafasi ya tano kwenye mbio za London Marathoni.

Advertisement