Stand United, Simba patachimbika Uhai Cup

Wednesday June 13 2018

 

By MASOUD MASASI

PATACHIMBIKA ndivyo tunavyoweza kusema Stand United leo watakuwa na kibarua kigumu pale watakapowavaa Simba katika mchezo wa Ligi ya Uhai Cup unaochezwa katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dodoma.

Kundi hilo B lina timu za Singida United, Njombe Mji, Stand United na Simba ambapo klabu mbili zitakazokuwa na pointi nyingi ndizo zitakazofuzu robo fainali.

Stand United yenye alama sita watakuwa na kazi nzito ya kuhakikisha wanapata ushindi katika mpambano huo huku Simba ambao walichapwa na Njombe Mji wakihitaji kupata pointi tatu za kwanza.

Kocha wa Stand United, Athumani Bilali “Bilo” alisema  hakuna kingine wanachokitaka katika mpambano huo zaidi ya kupata ushindi ambao utawapeleka moja kwa moja katika hatua ya robo fainali.

Alisema mpaka sasa wana pointi sita ambapo amesema mikakati yao ni kushinda mechi zote tatu hivyo wamejipanga kuweza kuwatandika Simba kwenye mchezo huo.

Bilo alisema katika kuelekea mchezo huo wa leo wameamua kuhamisha kambi yao  kutoka kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma na sasa wamejichimbika mjini Dodoma  ili kuweza kufanya mazoezi yao kwa faragha.

“Tulikuwa tumeweka kambi hapa kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma lakini sasa tumeamua kurudi mjini na hii kwa sababu tunahitaji uhuru zaidi kwenye kufanya mazoezi yetu,” alisema Kocha huyo.

 

Advertisement