Tarimba afunguka nafasi ya Sportpesa madeni ya Yanga -2

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SportPesa Tanzania, Abbas Tarimb

Muktasari:

Leo Tarimba anakamilisha makala yake kwa kuzungumzia ushindani ndani ya Simba na Yanga na mikakati ya SportPesa katika kuhakikisha michezo inazidi kusonga mbele. Endelea naye.

JUZI Jumanne tulianza kuchapisha makala ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SportPesa Tanzania, Abbas Tarimba akielezea mambo mbalimbali ambayo kampuni yake imefanya katika kuinua michezo nchini.

Leo Tarimba anakamilisha makala yake kwa kuzungumzia ushindani ndani ya Simba na Yanga na mikakati ya SportPesa katika kuhakikisha michezo inazidi kusonga mbele. Endelea naye.

Ushindani Yanga na Simba

Tarimba anafichua kuwa ushindani uliopo baina ya Simba na Yanga una mchango mkubwa katika kuitangaza SportPesa na soka la Tanzania.

“Ushindani wao umesaidia kiukweli kuendeleza mpira wa miguu. Unaweza kuona msimu huu Simba na Yanga wameingia katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba waliweza kufika hatua ya robo fainali msimu uliopita.

Kwa hiyo mafanikio yote haya tunaona tumeshiriki kwa kiasi kikubwa kuyawezesha. Kwa hiyo hata mafanikio ambayo zimeyapata kwetu sisi yanatusaidia kwa kiasi kikubwa.

Zawadi zawapa hofu

Katika mambo ambayo SportPesa imekuwa makini nayo ni kujihusisha moja kwa moja na fedha ambazo imekuwa ikitoa kwa washindi wa ubashiri wa matokeo.

“Unajua hizo fedha ni za kwao. Tungependa kuwashauri sio kwamba, namna ya kuzitumia lakini ni kwenye dhana ya uwekezaji ili fedha hizo ziweze kuwasaidia. Matatizo yako sehemu mbili. Kwanza unapompa mtu fedha na kumshauri halafu asifanikiwe, anaweza kuja kukuambia ulinishauri vibaya na amepoteza fedha zake hivyo, naomba unilipe fedha zangu ambazo nimepoteza kwa kufuata ushauri wako.

Lakini, kingine tunaogopa kusikia mimi nimecheza, wakati nataka kucheza hajanishauri, lakini nimeshinda anakuja anataka kuniambia nizitumiaje. Kwa hiyo hatutaki kuonekana kama tunaweka vikwazo kwa mtu kutumia fedha zake.

Kwa hiyo kama mtu amekuja kwetu kuomba ushauri ambao, sisi hatuwajibiki kwa huyo mtu kuufuata, huwa tunawashauri sana,” alisema Tarimba.

Alisema kutokana na hilo, hawataki kujihusisha sana na kuwashauri watu juu ya matumizi ya fedha wanazopata baada ya kushinda kwani, mambo yakienda kinyume, wahusika wanaweza kukimbilia katika vyombo vya kisheria.

“Kikubwa tunachowaambia watumie fedha zao vizuri kwa sababu ile ni kama bahati ambayo inaweza isijirudie tena ingawa wanaoendelea kucheza wamekuwa wakiendelea kupata vilevile,” alisema Tarimba.

Wajiweka kando madeni Yanga

Changamoto ya madeni ya mishahara na stahiki nyingine imesababisha baadhi ya wachezaji wa Yanga kuandika barua ya kuvunja mikataba na wengine kuidai klabu hiyo.

Hata hivyo, pamoja na SportPesa kuwa mdhamini ambaye pindi klabu inapozungumzwa kwa mtazamo hasi nayo inaathirika kwa namna moja au nyingine, Tarimba amedai hawahusiki na masuala ya ndani ya klabu.

“Sisi tuna wajibu fulani nao ni kuhakikisha fedha tunazopeleka zinatumika kwa mujibu wa makubaliano. Sisi huwa tunalipa kila baada ya miezi mitatu na kabla hatujalipa tena huwa tunahitaji vitabu vya hesabu vilivyokaguliwa,” anasema Tarimba.

“Hivyo wanatayarisha hesabu kuonyesha fedha tulizowapa wamezitumia kwa namna gani hivyo, kutokana na hilo tunapata nguvu ya kuwalipa tena. Kama kuna vitu tunaona haviko sawa tunayo nguvu ya kuhoji matumizi, lakini hadi sasa hatujakutana na hali kama hiyo.

“Sasa yawezekana klabu hizo zikawa na matumizi makubwa kiasi ambacho bili ya mshahara ikawa inazidiwa, hilo linakuwa ni tatizo la kiuongozi hivyo SportPesa haiwezi kuingia jikoni na kuanza kuelekeza.”

Uongozi mpya Yanga

Tarimba anaamini uongozi mpya wa Yanga utaifanya klabu hiyo iwe imara zaidi, jambo ambalo litaifaidisha klabu na SportPesa.

“Kwa maana ya uimara ni kweli. Uongozi mpya nadhani utaifanya Yanga kuwa sawa kwa sababu hali ya utulivu imeshaanza kuonekana,” alisema Tarimba.

Sakata la Kenya

Tarimba anasema kujiondoa kwa SportPesa katika kufanya shughuli zake nchini Kenya ni matokeo ya kutokuwa na uelewa mpana kuhusu ubashiri wa matokeo.

“Kilichotokea Kenya ndio kile nilichoeleza mwanzo kwamba, watu wanadhani kuwa kampuni za ubashiri wa matokeo zinaingiza kiasi kikubwa cha fedha na kwamba, pale wanaweza kutoza kodi nyingi bila kufahamu kwamba zinasaidia kukua ama zinafanya uendeshaji unakua mgumu?

Lakini, hapa Tanzania tumekuwa tukikutana mara kwa mara na Bodi ya Michezo ya kubahatisha na TRA na tunakwenda sawa. Juzi tumeambiwa makusanyo ya kodi kwa mkoa wa Ilala, shughuli hizi za ubashiri wa matokeo zinachangia 10% ya makusanyo yote kwa mwezi.

Hii inaonyesha kuwa shughuli hizi zina mchango mkubwa kwa kuchangia mapato ya Taifa,” alisema Tarimba.