Tenga aanguka, Kigogo CAF aenguliwa

Muktasari:

Tenga amehudumu nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF kwa muda wa miaka nane (8) tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2011

RAIS wa zamani wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na Shirikisho la Soka (TFF), Leodgar Tenga ameshindwa kutetea nafasi yake ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka (CAF) katika uchaguzi uliofanyika jana jijini Cairo.
Tenga aliyehudumu kwenye nafasi hiyo kwa miaka nane akiwakilisha Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, alishindwa kufua dafu mbele ya Rais wa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Moses Magogo ambaye aliibuka mshindi.
Katika uchaguzi huo ambao ulienda sambamba na Mkutano Mkuu wa CAF, Tenga alipata jumla ya kura 19 wakati Magogo aliyeibuka mshindi alivuna kura 33.
Tenga alikuwa akiwania nafasi ya ujumbe wa kuteuliwa kuwakilisha ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa mara ya tatu baada ya kuhudumu nafasi hiyo kwa miaka nane  (8) tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2011.
Katika Uchaguzi huo, Abdulhakim Al Shalmani wa Libya aliibuka mshindi wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji akiwakilisha kanda ya Kaskazini baada ya kupata kura 29 akimshinda Amar Bahloul wa Algeria aliyepata kura 21, Mohamad Ally Sobha wa Mauritius aliibuka mshindi kwa Kanda ya Kusini akiwashinda Adam Mthetwa, Andrew Kamanga, Elvis Raja Chetty na  Felton Kamambo.
Katika hatua nyingine Rais wa Shirikisho la Soka Nigeria (NFF), Amaju Melvin Pinnick ameondolewa nafasi yake ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa CAF katika mkutano huo uliofanyika jana.
Hakukuwa na sababu za kuondolewa kwa Pinnick nafasi hiyo ambayo sasa inashikiliwa na Constant Omar wa DR Congo wakati Rais wa Chama cha Soka Afrika Kusini (SAFA), Danny Jordaan amepanda kuwa Makamu wa Pili wa Rais na Faouzi Lekjaa wa Morocco atakuwa Makamu wa Tatu wa Rais.