Uzoefu waiponza Mauritania AFCON

Muktasari:

  • Timu ya Mauritania inayoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa mara ya kwanza, imekutana na kipigo kikali baada ya kunyukwa mabao 4-2 na Mali.

Cairo, Misri.Mashabiki wa Mauritania walikuwa na shauku ya kuiona timu yao ikipata matokeo mazuri katika mechi yake ya kwanza ya Fainali za Kombe la Afrika dhidi ya Mali.

Hata hivyo, ndoto yao ilizimwa baada ya Mauritania inayoshiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza katika historia yake, baada ya kukutana na kipigo cha mabao 4-1.

Mali yenye uzoefu na mashindano ya kimataifa ikiundwa na kundi kubwa la wachezaji wanaocheza Ulaya, ilipata matokeo hayo yaliyotarajiwa na wengi.

Wachezaji wa Mauritania walionyesha wana kitu lakini uzoefu katika mashindano makubwa kama hayo uliwaangusha na kuruhusu idadi kubwa ya mabao katika mchezo huo wa juzi usiku.

Matokeo hayo yameiweka Mali kileleni katika msimamo wa Kundi E  ikiongoza kwa pointi tatu ikifuatiwa na Angola, Tunisia ambazo kila moja imeweka kibindoni pointi moja huku Mauritania ikiburuza mkia kwa kutokuwa na pointi.

Abdoulay Diaby alifunga bao la kwanza kwa kiki kali ya umbali wa yadi 25 kabla ya Moussa Marega kuongeza la pili kwa mkwaju wa penalti.

Nyota wa Monaco Adama Traore alifunga bao la tatu kabla ya Moctar Sidi El Hacen kuifungia Mauritania kwa penalti.

Nyota mwingine anayecheza klabu ya Metz Adama Traore, alifunga bao la nne. Katika mechi nyingine, Ivory Cost iliigagadua Afrika Kusini bao 1-0 kabla ya Tunisia na Angola kutoka sare 1-1.