VIDEO: Bongo Zozo:Mama yangu aliangua kilio Samatta kujiunga Aston Villa

Muktasari:

Katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu England, Samatta aliipachikia bao Aston Villa licha ya mchezo wake huo wa kwanza klabu yake kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Bournemouth

Dar es Salaam. Shabiki wa kutupwa wa timu ya taifa ya Tanzania, Nick Reynolds ‘Bongo Zozo’, amesema mama yake aliangua kilio baada ya kusikia nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kujiunga na Aston Villa ya Ligi Kuu England.

Bongo Zozo hivi karibuni ameteuliwa kuwa balozi wa Utalii, alisema kuwa mama yake alikuwa na matarajio kuwa huenda Samatta atatua Norwich au West Ham United ambazo zipo karibu na nyumbani kwake.

"Unajua mama yangu anampenda sana Samatta, alipenda apate timu ya karibu na nyumbani ili akiwa na muda awe anakuja nyumbani kututembelea, lakini ilibidi akubaliane na uhalisia. Alilia kabisa yani machozi yalimtoka," alisema Bongo Zozo.

Shabiki huyo ambaye mke wake ni Mtanzania, alisema pamoja na mama yake kutofurahia, alikunjua nafsi na siku chache baadae wakapigiwa simu na Samatta na kuongea naye mawili matatu kabla ya kucheza mchezo wake wa kwanza.

Baada ya kuongea naye, Bongo Zozo aliweka mipango na kwenda kufanya fujo katika mchezo wake wa kwanza ambao ulikuwa na hatua ya nusu fainali ya Kombe la Ligi 'Carabao' dhidi ya Leicester City, "Nilifanya fujo na watanzania wengine, ule ni mwanzo tu, nasubiri fainali ya Wembley kwa hamu."

Katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu England, Samatta aliipachikia bao Aston Villa licha ya mchezo wake huo wa kwanza klabu yake kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Bournemouth ambao walimaliza pungufu kutokana na mchezaji wao mmoja kuonyeshwa kadi mbili za njano, nyekundu ikafuata.

Bongo Zozo ni mzaliwa na Zimbabwe mwenye raia wa Uingereza na mapenzi makubwa na Tanzania, akiwa England alisomea lugha ya Kiswahili kabla ya kuja nchini kwa mara ya kwanza na kujishughulisha na biashara ya kuuza kuku.

Kwa namna alivyokutana na Mama watoto wake na mengine kuhusu Bongo Zozo kuna sehemu ya kwanza na Pili katika mahojiano malum ambayo tumekuwekea katika Channel yetu ya Youtube, MCL Digital.