Mkuu wa Mkoa Manyara kuwapeleka vijana 50 KIA Marathon

Muktasari:

  • Vijana hao watakwenda kuuwakilisha mkoa wao na ili kuhakikisha wanarudi na medali, mkuu wa mkoa huo amekuwa mstari wa mbele kuwasaidia.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera amesema atawasafirisha wanariadha 50 kutoka mkoani humo kwenda kushiriki mbio za Kilimanjaro International Airport Marathon zitakazofanyika Novemba 19 mwaka huu mkoani Kilimanjaro.

Bendera aliongeza kuwa moja ya mikoa inayoipa sifa Tanzania katika medali ya kimataifa ni Manyara kupitia mchezo huo, hivyo atatumia nguvu zake kuwasapoti vijana waliokuwa tayari kujiajiri kwenye riadha hasa Manyara.

“Vijana wapo tayari kwa Kupambana na unapokuwa na vijana ambao wapo tayari kujisaidia hakuna budi na sisi viongozi kuwasapoti pale inapowezekana tena sio lazima uwape fedha bali kuwapa fulsa zinapotokea,” alisema Bendera.

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya KADCO, Hassan Kibelloh ambao ndio waandaaji wa mashindano alisema kuwa wameamua kujikita katika michezo ikiwa ni moja ya njia ya kujitangaza kwenye huduma yao.

 

“Wananchi wajue kuwa Marathon hii ambayo ni mara ya kwanza kufanyika yatakuwa ni ya kila mwaka na kila mtu anakaribishwa kushiriki na hii itawasaidia vijana kuonesha vipaji vyao lakini kujitangaza pia na katika mataifa mbalimbali,” alisema Kibelloh.

 

Mshindi wa kwanza katika mbio hizo zilizogawanyika katika Makundi matatu, Km 5, km 21 na km 42 atajinyakulia kitita cha Sh5 milioni kwa km 42 na mshindi wa kumi akiondoka na Sh1 milioni.