Wambura akwaa kisiki, aendelea kusota rumande

Dar es Salaam. Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Michael Wambura, anaendelea kusota rumande, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, kutupilia mbali pingamizi lililowasilishwa na upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mshtakiwa huyo.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina baada ya kupitia hoja za pande zote zilizowasilishwa mahakamani hapo.

Wambura alifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza, Jumatatu Februari 11, mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya Sh100milioni.

Wambura baada ya kusomewa mashtaka, hakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kutokana na hali hiyo, Wakili wake, Majura Magafu aliwasilisha pingamizi mahakamani hapo, akiiomba kutupilia mbali kesi hiyo kwa sababu mashitaka yote 17, hayajafunguliwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi.

Magafu alidai kesi hiyo ilipaswa kufunguliwa kama kesi ya kawaida ya jinai ambayo inamruhusu mshitakiwa kujibu mashtaka yake.

Pia Majura, alidai katika maudhui ya hati ya mashtaka hakuna hata kosa moja la uhujumu uchumi kama ilivyoainishwa.

Magafu alidai kwa mujibu wa kifungu cha 129 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai( CPA) kinaipa mamlaka Mahakama hiyo kukataa kusajili kesi, endapo zina makosa, lakini pia kupitia kifungu hicho kinaipa mamlaka mahakama husika kuikataa na kuitupilia mbali kesi husika.

Akisoma uamuzi huo, Mhina alisema, kifungu cha 3 cha Sheria ta Uhujumu Uchumi, kinaondoa Mamlaka ya Mahakama ya Kisutu, kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi, isipokuwa DPP atakapowasilisha kibali cha kuiruhusu mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.

Mhina alisema Mahakama ya Kisutu, ina Mamlaka ya kumsomea mshtakiwa mashtaka yake pamoja na maelezo ya mashahidi na vielelezo na sio vinginevyo.

“Mahakama ya Kisutu imefungwa mikono, haina Mamlaka ya kuondoa au kufanya maamuzi yoyote katika hati hii ya mashtaka, mpaka itakapopata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) cha kuruhusu kesi hii kusikilizwa hapa” alisema Hakimu Mhina na kuongeza

“ Hivyo mahakama hii haina mamlaka ya kuondoa kesi na kwamba masuala ya kisheria yaliyowasilishwa na upande wa utetezi yanatakiwa kuelekezwa katika mahakama yenye mamlaka ambayo ni Mahakama Kuu,” alisema Hakimu Mhina.

Hakimu Mhina baada ya kueleza hayo, alisema upande wa utetezi kama hawajaridhika na uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kisutu, wanaweza kukata rufani Mahakama Kuu.

Hakimu Mhina baada ya kutoa uamuzi huo, aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 28, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa alirudishwa rumande kutoka na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana.

Awali, kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo, Wakili wa Serikali Ester Martin alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya mahakama kutoa uamuzi na wako tayari kwa ajili hiyo.