Breaking News

Yanga ikipewa RS Berkane, Al-Masry pagumu ila Bandari, Zanaco patamu CAF

Wednesday October 9 2019

 

By CHARLES ABEL

Dar es Salaam. Wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga leo itamjua mpinzani wake katika kusaka kufuzu kwa hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Droo ya hatua hiyo ya mchujo ya Kombe la Shirikisho imepangwa kuchezeshwa leo Oktoba 9 jijini Cairo, iwapo Yanga itafanikiwa kushinda mechi zake mbili za mtoano itafuzu kwa mara ya tatu kucheza hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Yanga imeingia katika hatua hiyo baada ya kung'olewa na Zesco United ya Zambia katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa jumla ya mabao 3-2.

Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) zinazosimamia mashindano hayo, timu 16 zilizotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika zitaumana na timu 16 zilizotinga hatua ya mchujo ya Kombe la Shirikisho, ili kusaka timu zitakazocheza hatua ya makundi.

Tayari timu 16 zilitolewa kwenye Ligi ya Mabingwa zimeshajulikana ambazo ukijumuisha na Yanga, nyingine ni UD Songo (Msumbiji), Côte d'Or (Shelisheli), Green Eagles (Zambia),  Fosa Juniors (Madagascar),  Elect-Sport (Chad), KCCA (Uganda), Asante Kotoko (Ghana), FC Nouadhibou (Mauritania), Generation Foot (Senegal), Cano Sport (Guinea ya Ikweta), Gor Mahia (Kenya), ASC Kara (Togo), Horoya (Guinea) na Al Nasr (Libya).

Timu 16 ambazo zimetinga hatua ya mchujo ya Kombe la Shirikisho ni RS Berkane (Morocco), Al-Masry (Misri), Hassania Agadir (Morocco), Zanaco (Zambia) na Enugu Rangers (Nigeria ).

Advertisement

Nyingine ni Djoliba (Mali), Paradou AC (Algeria), ESAE (Benin), DC Motema Pembe (DR Congo), FC San Pedro (Ivory Coast),Pyramids (Misri), Bandari (Kenya), Bidvest Wits (Afrika Kusini), TS Galaxy (Afrika Kusini), Proline (Uganda) na Triangle United (Zimbabwe).

Vigogo hivi Yanga ijipange

Tofauti na awamu zilizopita, safari hii kunaonakana hakuna idadi kubwa ya timu tishio katika Kombe la Shirikisho jambo ambalo pengine lingeiweka Yanga kwenye presha kubwa.

Hakuna utitiri wa timu kutoka Kaskazini mwa Bara la Afrika lakini hata zile za Ukanda huo ambazo zimefanikiwa kuingia kwenye hatua ya mchujo, hazina rekodi ya kutisha pindi zinaposhiriki mashindano ya kimataifa.

Hata hivyo bado kuna timu ambazo zinaweza kuwa kikwazo kwa Yanga iwapo zitapangwa nazo kutokana na uwekezaji mkubwa zilizofanya, ubora wa vikosi vyao pamoja na uzoefu zilizonazo kwenye mashindano ya kimataifa.

Timu hizo ni Al Masry, Paradou, Pyramids FC, DC Motema Pembe, Djoliba, Hassania Agadir, Enugu Rangers na RS Berkane.

Al Masry waliwahi kutinga hatua ya fainali ya mashindano hayo mwaka 2018 kama ilivyo kwa RS Berkane iliyofanya hivyo msimu uliopita. Hassania Agadir yenyewe ilitinga hatua ya robo fainali pia kwenye msimu uliopita.

Enugu Rangers yenyewe imeshaonja ladha ya kutwaa taji la Afrika ikifanya hivyo mwaka 1977 ilipotwaa Kombe la Washindi lakini pia imeshawahi kutinga hatua ya fainali, nusu fainali, robo fainali na makundi mara nyingi.

Lakini kingine ni uwekezaji mkubwa wa fedha uliofanywa na timu hizo katika kusuka na kuandaa vikosi vyao na hapo pia unazikuta timu kama Djoliba, Paradou na Pyramids FC.

Yanga ikikomaa hapa inapenya

Lakini ukiondoa timu hizo zinazoonekana zinaweza kuwa tishio kwa Yanga, zipo nyingine ambazo wawakilishi hao wa Tanzania wana msuli wa kutosha kupambana nazo ambazo ni Proline (Uganda), Bidvest Wits na TS Galaxy (Afrika Kusini), Bandari FC (Kenya), Zanaco (Zambia), Triangle United (Zimbabwe), San Pedro (Ivory Coast) na ESAE ya Benin.

Kiwango cha uzoefu na mafanikio kwenye mashindano ya Afrika ambacho Yanga wamekuwa nacho, kinaweza kuwa silaha tosha kwa wawakilishi hao wa Tanzania kupata ushindi dhidi ya timu mojawapo ikiwa ikipangwa nayo lakini bado inapaswa kujiandaa kikamilifu.

 

Rekodi inavyoibeba Yanga

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Yanga imetinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mara mbili kwa kupenya kupitia mechi za mchujo mara baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mwaka 2016 iliitupa nje Sagrada Esperanca ya Angola kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 na mwaka 2018 iliitoa Welayta Dicha ya Ethiopia kwa ushindi kama huo.

Vita sio nyepesi

Matokeo ya kushangaza kwenye mashindano ya klabu Afrika msimu huu yanapaswa kuipa fundisho Yanga na kujiandaa kikamilifu kucheza hatua hiyo ya mchujo kama kweli ina nia ya dhati ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Timu nyingi zinaonekana kujiandaa vizuri na ikiwa itakuwa na maandalizi ya wastani, Yanga inaweza kujikuta inashindwa kutinga kwenye makundi

Advertisement