Yanga yamtupia virago Molinga kimyakimya

Saturday January 11 2020

 

Dar es Salaam. Mshambuliaji David Molinga aliyekuwa akicheza Yanga kwa mkopo ndio basi tena baada ya mabosi wa Yanga kuafiki kuachana naye ili kusajili wachezaji wengine wanaooamini wataisaidia timu hiyo kwa nidhamu ya hali ya juu.

Molinga aliyetibuana na viongozi wa kitendo alichokionyesha alipofanyiwa mabadiliko katika mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara, imefanya awe ni mchezaji wa tano aliyesajiliwa na Kocha Mwinyi Zahera kutimka Jangwani, baada ya Sadney Urikhob, Juma Balinya anayetajwa kutua Gor Mahia ya Kenya, Issa Bigirimana na Maybin Kalengo.

Molinga anaondoka akiwa amefunga mabao manne katika Ligi Kuu Bara na kinara wa ufungaji wa Yanga akisaidia timu hiyo kupanda hadi nafasi ya 5 katika msimamo.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema wapo kwenye mazungumzo ya kuvunja mkataba na Molinga aliyeshindwa kufikia malengo kwa mujibu wa mkataba wake wa miaka miwili akitokea kwao, DR Congo.

“Mbadala wa Molinga atajulikana kwani bado tuna nafasi na tunaendelea kusaka mchezaji ambaye anaweza kuwa msaada kwenye kikosi chetu ambacho kinahitaji maboresho kabla ya dirisha kufungwa,” alisema Mwakalebela.

Naye Kocha Mpya wa Yanga, Luc Eymael juzi usiku hakufurahishwa na hatua ya timu yake kung’olewa Kombe la Mapinduzi, akisema hataki kuona timu inadharauliwa.

Advertisement

Kocha huyo anayejiandaa kusaini mkataba wa miezi 18  alisema hakuelewa kwanini Yanga haikupanga kikosi kamili katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Mtibwa Sugar na kujikuta waking’olewa kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1.

Raia huyo wa Ubelgiji alisema alitegemea katika hatua ambayo timu ilifikia alitaka kuona kikosi kamili kikitumika na sio kujaribu lengo likiwa kulinda jina na heshima ya klabu hiyo kongwe nchini.

Alisema hataki kuona Yanga inaidharau timu yoyote pinzani na kila mchezo kwao utakuwa na uzito mkubwa.

Aidha alibainisha kwa wachezaji aliowaona jana na sasa anataka kuzungumza nao kabla ya kuzungumza katika vyombo vya habari.

Alisema atakutana rasmi na nyota wake mara baada ya kurejea jijini Dar es Salaam leo tayari kwa mikakati ya kuanza kazi kwa kasi katika ajira yake mpya hiyo.

Advertisement