Yanga yafanya umafia yamvuta Kotei Jangwani

Saturday January 11 2020

 

HAO Yanga wanachokifanya kwa sasa ni kama sifa. Kwani namna wanavyosuka kikosi chao, basi wapinzani wao wajipange mapema. Unaambiwa mara baada ya kumshusha Kocha Mpya kutoka Ubelgiji akiwa na rekodi za kibabe, sasa Yanga wanapeleka mshtuko Msimbazi wakiwa hatua ya mwisho kumshusha kiungo aliyewapa heshima Wekundu hao.

Yanga wakati wowote kuanzia leo Jumamosi watamshusha nchini kiungo mkabaji Mghana, James Kotei raia wa Ghana, ambaye kuachwa kwake Msimbazi kulizua gumzo kwa mashabiki wa klabu hiyo wanaoendelea kumuota kwa kazi aliyoifanya misimu aliyoichezea timu yao.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imepenyezewa ni kwamba kigogo anayemsaidia Bilionea Ghalib Mohamed anayeisajilia Yanga, Mhandisi Hersi Said ndiye aliyekamilisha dili hilo muhimu katika kikosi hicho cha Jangwani.

Kumbuka, Hersi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya klabu hiyo alikuwa  Afrika Kusini kukamilisha mazungumzo na kocha wao mpya, Luc Eymael na baada ya kila kitu kumalizika kwa kocha huyo haraka usajili ukaanza.

Dili la Kotei likatua mezani kwa Eymael ambaye alimpitisha kiungo huyo na haraka Hersi akatua klabu ya Kaizer Chiefs anayoichezea kiungo huyo kukamilisha kila kitu.

Katika mazungumzo hayo mbali na Yanga kumalizana kila kitu kuhusu Kotei, pia bosi huyo akiwa na yule wa Kaizer, Bobby Motaung waliingia makubaliano ya ushirikiano pande hizo mbili.

Advertisement

Usajili huo huenda ukaipa nguvu zaidi Yanga katika kukisuka kikosi chao ambapo lengo kubwa ni kuhakikisha wanachukua ubingwa.

Mapema jana Hersi ambaye kampuni yao ya GSM ndio iliyodhamiria kuisuka Yanga, aligoma kuzungumzia usajili huo aliliambia Mwanaspoti kuwa wako katika malengo makubwa katika kuirejesha Yanga tishio itakayosumbua hapa nchini na nje ya Afrika.

“Kama kuna mtu anadhani tunatania atajijibu mwenyewe tunasuka timu, siku zote tunataka watu watambue kwamba tupo Yanga kuhakikisha tunairejesha heshima ya timu hii kwa hapa ndani na nje ya Afrika tutazungumza kwa vitendo zaidi,” alisema Hersi.

Mwanaspoti linafahamu jana mchana Kaizer lilimuita meneja wa Kotei ili kuhakikisha anampeleka kiungo huyo Yanga haraka.

‘Amakhosi’ndio wanaommliki Kotei na kiungo huyo bado hajafanikiwa kuonyesha uwezo mkubwa tangu atue hapo kama mchezaji huru akitokea Simba.

Kabla ya kutua Amakhosi, Kotei alikuwa mmoja wa nguzo muhimu katika kikosi cha Simba akiisadia timu hiyo kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita huku akicheza karibu mechi zote.

Hata hivyo, Simba haikumuongezea mkataba licha ya kuibuka kiungo bora ndani ya timu hiyo huku mashabiki nao wakionyesha kutokukubaliana na kuachwa kwa Mghana huyo.

Advertisement