Yanga yamweka chini Kabwili tuhuma za kupewa rushwa na Simba SC

Muktasari:

Kabwili alisema hayupo tayari kuzungumzia suala hilo kwasasa ameiachia kamati iliyopewa jukumu la kufanya uchunguzi ifanye kazi yake.

Dar es Salaam.Uongozi wa klabu ya Yanga leo unatarajia kukutana na kipa wake namba tatu, Ramadhani Kabwili kwaajili ya kupata ufafanuzi kuhusiana tuhuma alizozitoa za kupewa hongo klabu ya Simba.

Kabwili jana akihojiwa na mmoja ya redio jijini Dar es Salaam alidai kufuatwa na viongozi wa Simba na kumtaka kumpa hongo ya gari aina IST ili apate kadi mbili za njano zitakazomfanya asicheze dhidi ya mabingwa hao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Fredrick Mwakalebela alisema wako pamoja na mchezaji huyo lengo ni kuona jambo hilo linafika mwisho na ukweli kujulikana.

"Mbali na kusikia taarifa za mchezaji huyo pia tumeona taarifa kutoka Shirikisho la Soka Tanzania 'TFF' wakiitaka kamati ya nidhamu ilifuatilie kama linaukweli na sisi tunafanya mazungumzo na mchezaji kutuhakikishia hilo kama linaukweli," alisema Mwakalebela.

"Lengo la kufanya hivyo ni kutaka kufahamu ukweli na kama ni kweli itakuwa ni moja ya njia ya kuboresha malalamiko mbalimbali kwenye soka letu," alisema Mwakalebela.

Wakati huohuo Kabwili alisema hayupo tayari kuzungumzia suala hilo kwasasa ameiachia kamati iliyopewa jukumu la kufanya uchunguzi ifanye kazi yake.

"Sina cha kuzungumza kwa sasa nawaachia viongozi waliopewa jukumu la kufanya uchunguzi mambo yakiwa sawa nitaweza kuzungumza lolote au litazungumzwa na kamati husika," alisema Kabwili.