Soudy Brown, Maua Sama wasota rumande

Wednesday September 19 2018

 

By Rhobi Chacha

Dar es Salaam. Mwimbaji wa kike anayetamba na wimbo ‘Iokote’ Maua Sama na mtangazaji wa kipindi cha Shilawadu maarufu ‘Soudy Brown’ wanaendelea kusota rumande tangu walipokamatwa Jumapili Septemba 16, mwaka huu.

Wasanii hao walikamatwa sambamba na meneja wa Maua aitwaye, Fadhili Kondo, na wanashikiliwa kwa kosa la uharibifu wa mali ya umma baada ya kuonekana mtandaoni wakirusha hela na kuzikanyaga.

Msemaji wa nyumba ya vipaji ‘Tanzania House of Talent’ Rehema Jones amesema,  mpaka sasa watu hao bado wanashikiliwa na jeshi la polisi.

Alipoulizwa kuhusu maendeleo yao na iwapo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani, Rehema amesema: “Utaratibu ndiyo unafanyika kuhusu suala la mahakama  na sisi tunasubiri kuona nini kitaendelea kwa sasa hatuna zaidi cha kuzungumza.”

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu idadi ya wasanii ambao inasemekana wameendelea kukamatwa kufuatia sakata hilo, Rehema amesema: “THT ina taarifa za watu watatu tu, hao wengine hatuwezi kuwazungumzia.”

Watatu hao walikamatwa katika Kituo cha Polisi Kinondoni kabla ya kuhamishiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Central.

Advertisement