Ali Kiba ataja sababu za kuchukia maisha ya kuigiza

Monday September 2 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi

Dar es Salaam. Msanii wa muziki wa bongo fleva nchini Tanzania, Ali Kiba amesema anaweza kuishi maisha ya kuigiza lakini hapendi.

Ali Kiba ametaja sababu za kutofanya hivyo.

Kiba ameyasema hayo jana Jumapili Agosti 01,2019 katika uzinduzi wa filamu ya 'Siyabonga' ya msanii Gabo itakayoanza kuonyeshwa katika mtandao wa Swahiliflix, hafla iliyofanyika mlimani City Jijini Dar es Salaam.

 Msanii huyo alijikuta akiyasema hayo pale alipoulizwa amewezaje kutofautisha maisha ya kifamilia na ya kazi yake ya sanaa.

 Katika maelezo yake, mkali huyo wa kibao cha Seduce, Kadogo na Aje, alisema sio kwamba maisha ya kuigiza hayajui ila akiamua kuyafanya watu wataogopa na kila saa kamera za waandishi zitakuwa kwake isipokuwa hapendi tabia hiyo.

 Pia alisema hapendi kuishi maisha ya kuigiza kwa kuwa anaiogopa kesho na kubainisha kuwa hakuna binadamu anayejua kesho yake itakuwaje.

Advertisement

 Sababu nyingine Ali Kiba alisema huwa anafurahia kuishi maisha ya kawaida kama watu wengine na kuongeza anaamini ndiyo imemjengea heshima kubwa kwenye jamii. 

 Wakati kuhusu filamu ya 'Siyabonga' alivyoiona,  alisema ni nzuri na kutoa ushauri kwa wasanii kushikamana ili kuweza kufika mbali.

 "Wasanii wanapaswa kushikamana kama ngumi lakini sasa hivi ninavyoona wapo wametawanyika kwa kufanya hivyo sanaa hii haitafika mbali tunapotaka," alisema Ali Kiba.

 

Advertisement