Maua Sama: Nilipowekwa mahabusu, familia yangu haikutaka nijihusishe na muziki

Wednesday September 4 2019

 

By Rhobi Chacha, Mwananchi

Dar es Salaam. Siku saba baada ya kuachia wimbo wake mpya uitwao 'Niteke' mwanamuziki nchini Tanzania, Maua Sama amefunguka kuwa familia yake ilikataa asifanye muziki tena.

 Maua ambaye amewahi kutamba na nyimbo kama Iokote, Nakuelewa amepiga stori na Mwananchi juzi Jumatatu Septemba 2,2019 alisema baada ya kupata matatizo ya kuwekwa rumande alihitaji kupata mapumziko kufanya muziki ambapo familia yake ilitaka aachane nao kabisa.

Septemba 17, 2018 Maua Sama alishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za uharibifu wa mali kwa kurusha fedha kisha watu kuonekana kuzikanyaga kanyaga kwenye video ya wimbo wake maarufu  ‘Iokote’

"Wimbo wa ‘Iokote’ ilitakiwa kuwa ni wimbo wa mwisho kwangu, kwani kutokana na ishu ya kuwekwa rumande wazazi wangu hawakutaka niendelee na muziki japo mimi mwenyewe nilitaka kupumzika tu kwa muda," alisema.

Maua alisema ilibidi akae chini na familia yake na kuweka sawa suala la yeye kuendelea na muziki na baada ya kuelewana nao ndipo alipoamua kutoa wimbo wake mpya wa ‘Niteke’.

 "Baada ya kutoa wimbo huu sasa nafikiria kutoa wimbo utakaohusu changamoto nilizopitia kwani tukio la kuwekwa rumande halitaweza kufutika kichwani mwangu," alisema.

Advertisement

 

 

Advertisement