RAHA, KARAHA ZA WASANII KATIKA ‘AWAMU YA TANO’

Muktasari:

Miaka mitano ya Rais John Pombe Joseph Magufuli inaisha Jumatano. Ni siku tano tu toka hii leo. Tutatangaziwa rais atakayeunda serikali mpya. Suala la mitano tena au mitano kwanza, liko mikononi mwa wapiga kura wa nchi hii. Yes!

Miaka mitano ya Rais John Pombe Joseph Magufuli inaisha Jumatano. Ni siku tano tu toka hii leo. Tutatangaziwa rais atakayeunda serikali mpya. Suala la mitano tena au mitano kwanza, liko mikononi mwa wapiga kura wa nchi hii. Yes!

Kwa miaka mitano inayoisha wiki ijayo tunabaki na kumbukumbu nyingi sana. Kuanzia kwenye siasa, michezo, sanaa na maisha ya kila siku kwa ujumla wake. Ilikuwa miaka mitano ya mshike mshike. Pambana au ufe njaa. Ndiyo!

Yale mazoea ya kidwanzi yalitoweka kama mahaba ya Mondi kwa Wema. Kuna michongo ilisimama kabisa. Wale wapigaji wa mjini walikosa fursa ya kupiga pesa za wajinga. Hata wadangaji ‘wamestrago’ mno kwa miaka mitano inayoisha.

Wazee wa Ngwasuma kwa Wana wa pale Makumbusho na Msasani. Twanga Pepeta wa Mango Garden na kule TCC Chang’ombe. Ilibaki kuwa ndoto tamu inayoumiza. Ubora na ushawishi wao kwa mashabiki ulisinyaa. Noma!

Sanaa na mtaa umepoteza watu wengi. Kwa ajali na vifo vya kawaida. Mzee Said Mabera mpiga gitaa wa Msondo Ngoma tangu na tangu. Hitimisho la pumzi zake lilikuwa ndani ya miaka mitano hii. Ndicho kilichotokea kwa King Majuto na wengineo.

Uso wa kiwanja cha kulia bata Katikati ya jiji. Naongelea Club kubwa ya kimataifa Bilcanas. Tulishuhudia uhai wake wa muda mrefu toka enzi za Mbowe Club, ukifikia ukomo au tamati kwa kuvunjiliwa mbali. Yes ilikuwa alama ya Dar es Salaam.

Hata sanaa ya filamu ilitetereka sana. Kwa miaka hii mitano hakukuwa na ule mzuka kisanaa. Yawezekana mazoea yaliwaponza. Na biashara kuwatia upofu na kushindwa kwenda na kasi ya mfumo wa kodi mbele.

Achana na hayo makitu. Vipi umaarufu wa mtu kama Wema Sepetu? ‘Ofu kozi’ ulimezwa na matukio yake ya mapema ndani ya miaka hii mitano ya Magu. Kesi na muingiliano wa maisha ya kisiasa akajikuta nje ya ‘meinistrimu’.

Hamisa Mobetto, Nandy, Zari, Shishi Baby na wengineo. Ni wanawake wa mjini wenye umaarufu ambao walienda sawa na miaka mitano ya Magufuli. Waliendelea kukimbiza mitandaoni na mitaani licha ya mtaani watu kulia ukata.

Sifa za pekee zinaenda kwa Elizabeth Michael ‘Lulu’, akili kubwa ndani ya mwili mdogo. Pamoja na uwepo wake kwenye mikono ya watu salama. Lakini hata yeye binafsi aliweza kuhimili presha zake za maisha ya umaarufu.

Alikwenda jela kutumikia kifungo. Kwa bahati njema akatoka kwa msamaha wa rais. Aliporudi mtaani akaweka pozi kwa utulivu mkubwa. Mashauzi na vituko vya hapa na pale aliweka kando. Yes hii kitu ilimsaidia sana.

Pamoja na ugumu wa soko la filamu. Lakini akabaki kuwa alama ya ‘gemu’ lote la Bongo Movie. Ikiwa ni pamoja na ubalozi wake kwa taasisi kadhaa na bidhaa za kibiashara. Huku penzi lake kwa Majizzo akilimiiki kinyama.

Kuwa mpenzi wa Majizzo ni moja. Kumiliki penzi la Majizzo ni jambo lingine kubwa. Kuna kina Majizzo wengi mitaani, na kuna kina Lulu wengi sana mitaani. Ni akili kubwa iliyomtuliza Lulu na akili kubwa iliyomtuliza Majizzo.

Watu sampuli yao kwa maana ya wenye umaarufu. Wengi walishindwa kudumu Katika uhusiano. Tunamuongelea mtu ambaye alikuwa na Hamisa Mobetto kabla ya Lulu. Na Lulu alikuwa na wengineo kabla ya Majizzo.

Miaka hii mitano ya Magufuli inabaki kwenye kumbukumbu nzuri kwa baadhi ya mastaa. Na kumbukumbu mbaya kwa baadhi yao. Shishi Baby ‘Shilole’, hawezi kubaki na kumbukumbu nzuri katika uhusiano wake.

Kipigo cha kikatili toka kwa ustaadhi Uchebe, kilihitimisha ndoa yao rasmi. Ndivyo ilivyo kwa Zari na Hamisa ake. Ambao wote walitemana na msela wao wa Tandale Mondi Bin Laden. Kimapenzi ‘ofu kozi’. Yes!

Vipi kuhusu mapedeshee? Wale ambao walimwaga pesa kindezi kwenye kumbi za starehe? Hawapo tena, muziki wa dansi ni kama waliushikiliwa wao tu. Maana mirija yao ilipokatwa na bendi zikakosa nguvu.

Kuna chimbo za wapenda starehe pia zilikosa msisimko kwa miaka hii mitano. Kama Sinza, maeneo ambayo ungepata pisi kali .Bongo michongo ilidorora. Pesa za kuchezea zilikosa urafiki na mifuko ya wala bata mjini. Kifupi nidhamu ya uzinzi na uasherati iliota mizizi.

Kilichoendelea ni utulivu wa ndoa nyingi. Na pia kudorora kwa ndoa nyingi. Kuna waliokosa pesa za kuchezea waliishia kutulia kwenye ndoa. Na kushindwa kumiliki pisi za bata. Njaa ikawatuliza ndani kama wana kondoo kwenye mazizi.

Lakini wapo ambao walipokosa michongo ya pesa za kutafuna hovyo. Wakakimbiwa na wapenzi wao. Ndiyo! Mwanamke uliyempata kwa pesa pia atakuacha kwa pesa hizo hizo. Ndivyo ilivyo katika uso wa dunia hii.

Tofauti yake ni kwamba ulimpata kwa sababu ya wingi wa pesa zako. Na Sasa anakuacha kwa sababu ya uchache wa pesa zako. Madikteta husema kwamba “walivyoingia madarakani ndivyo watakavyotoka.

Huwezi kumtoa dikteta aliyeingia kwa mtutu ukitumia karatasi. Pia totozi uliyempata kwa nguvu ya pesa, pia atakuacha kwa nguvu ya pesa hiyo hiyo. Michongo ya kijanja mjini imetoweka na pisi flan hivi amazing zimetoweka.

Tutakutana Jumamosi ijayo tukiwa na serikali mpya. Yes Jumatano twende zetu tukapige Kura kuchagua mtu tunayemtaka. Mitano kwanza au mitano Tena? Huo ni uamuzi wa mtu binafsi kwenye sanduku la kura.