Ali Kiba, Diamond wameuingia mtego wa kupoteza mashabiki

Sunday November 11 2018

 

SOMETIMES kama mbwai mbwai! Waziri wa Katiba na Sheria, Prof Palamagamba Kabudi, juzikati aliamua kama mbwai mbwai tu. Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, alimuuliza ‘maswali nchokonoe’ kuhusu kesi ambazo Serikali imefunguliwa kwenye mahakama za kimataifa zenye kutokana na migogoro ya uvunaji madini nchini.

Kabudi akamchenjia Zitto, “We we we, hilo swali lako la mtego sijibu. Halafu huo mtego kama ni wa kutumwa au bahati mbaya siuingii. Narudia tena kama ni mtego wa bahati mbaya au wa kutumwa sitauingia.” Hiyo nukuu ina nyongeza ya wino kidooogo!

Weusi wa mambo yao ukasababisha wao wawili watawale soko na gumzo la muziki Tanzania. Ikawa ni Diamond dhidi ya Kiba, nani zaidi? Na mashabiki wakajaa upande wao. Stori za bifu la Diamond na Kiba halihitaji maelezo mengi. Maana linajulikana kwa wino uliokolea.

Diamond anaongoza ngome kubwa ya kibiashara yenye jina la Wasafi, ambayo ni lebo ya muziki, inamiliki studio ya kurekodi, pia ni wasambazaji na wauzaji wa nyimbo. Wasafi wanamiliki televisheni, redio na tamasha kubwa la muziki, Wasafi Festival.

Kalenda ya Wasafi Festival inamwekamweka kwa sasa. Juzikati Diamond alipokuwa anatangaza ujio wa tamasha hilo, alitumia nafasi hiyo kumwalika Kiba ili naye ashiriki, akisema lengo ni kuupaisha muziki wa Tanzania.

Unajua nini? Wito wa Diamond ulikuwa mzuri, lakini mapokeo ya mashabiki yalibeba tafsiri ya mtego. Kwamba Kiba angekataa angeonekana ndiye mkorofi. Na maneno yalishaanza.

Watu wengi walitarajia Kiba angejibu kama Kabudi: “Huo mtego uwe wa bahati mbaya au wa kutumwa sitauingia.” Haikuwa hivyo, yalipita maneno mengi, lakini kauli ya Kiba ikajenga amani. Mapokeo chanya ya Diamond yakamaliza kila kitu. Hapa lazima wote wale kudoz za kutosha. Wametisha mno. Wameshinda.

MTEGO KILA UPANDE

Diamond kumwalika Kiba kwenye shoo ya Wasafi lilikuwa jambo jema. Hata hivyo, asiyetambua hilo, angeona bwana mdogo wa Tandale anapandisha mabega, kuwa yeye ni zaidi ya Kiba na anaweza kumlipa ili apige kazi Wasafi Festival.

Wanasema chuki ni upofu, upendo huona kila kitu. Kwamba Kiba angetanguliza chuki, asingeona uzuri wa Wasafi Festival wala heshima ya kumwalika ashiriki naye jukwaa moja. Alipoweka upendo mbele, akajua thamani ya mwaliko, kisha akajibu kwa nidhamu.

Kiba alipokea mwaliko na kuomba radhi kwamba ratiba yake ya kutangaza kinywaji chake cha MoFaya inambana, hivyo asingeweza kupanda jukwaani Wasafi Festival, lakini kwa malengo ya kukuza muziki, akaomba kudhamini shoo hiyo ya Wasafi. Narudia; chuki ni upofu, upendo huona kila kitu! Diamond angepumbazwa na chuki, asingeona nia njema ya Kiba kuipiga tafu ya kifedha Wasafi Festival, angeona Kiba alitaka kujifanya baabkubwa kuwa, ana fedha mpaka anamdhamini.

Upendo huona kila kitu, kwamba Diamond akaona tobo la mafanikio ya Wasafi Festival kupitia jeki ya MoFaya. Akakubali, akamwagiza meneja wake Sallam afanye mazungumzo na meneja wa Kiba, bi’dada Seven. Mpaka hapo wote wawili wakawa wameshinda sana. Na walikwepa mitego vizuri kabisa. Siwapingi wenye kusema uamuzi wa Diamond na Kiba una watu nyuma yao. Midomo mali yenu bana.

Wote wameonesha uungwana, ila hili usiache kuliona; ilikuwa rahisi Kiba kukataa kufanya shoo ya Wasafi kwa sababu angejibu kama alivyojibu kuwa ratiba haimruhusu na angeeleweka. Hata hivyo, Diamond asingeeleweka hata kidogo kama angekataa udhamini wa Kiba kupitia kinywaji chake cha MoFaya. Unakataaje udhamini? Kuna kushindwa kuafikiana kwenye vigezo na masharti ya udhamini, lakini siyo kukataa kwamba hutaki kudhaminiwa na Kiba. Yaani Diamond angeuchomolea udhamini wa MoFaya, angeonekana wa hovyooo!

Baada ya wote kushinda na kuvuka mitego sawia, naomba nitoe homework; je, MoFaya ikipita kama mdhamini mkuu wa Wasafi Festival, kisha masharti yakawa tamasha liitwe MoFaya Wasafi Festival itakubalika? Kwa vile MoFaya Afrika Mashariki inabeba jina la Kiba, vipi likiitwa Ali Kiba MoFaya Wasafi Festival?

WAMEPUNGUZA MASHABIKI

Mapatano ya kibiashara kati ya Diamond na Kiba yanagusa maeneo matatu; heshima, fedha na mashabiki. La kwanza kuhusu heshima ni kuwa heshima yao imeongezeka na kama watafika pazuri zaidi, itaongezeka zaidi. Wanaonekana wanakua sasa na wanayatazama maisha kuliko viburi vya majina, umaarufu na tambo za nani zaidi mbele ya mashabiki.

Fedha; wanakwenda kuzitengeneza. Kiba itampasa kutumbukiza fedha zake ili MoFaya ibebe thamani ya mdhamini wa Wasafi Festival. Hivyo, Diamond atapata fedha ambazo zinaweza kupunguza gharama za maandalizi ya tamasha hilo. Hiyo ni faida ya moja kwa moja.

Biashara ya vinywaji ina ushindani mkubwa Tanzania. Hasa vile vya kuongeza nishati ya mwili mithili ya MoFaya. Maana vipo vingi na vingine vimeteka soko kwa miaka mingi. Hivyo, inabidi MoFaya itangazwe hasa.Wasafi Festival ni tamasha kubwa. Diamond ni msanii mkubwa na anapendwa sana. MoFaya kutangazwa kupitia tamasha hilo, ambalo Diamond na wasanii wengine wakali wa lebo ya Wasafi kama Harmonize, Rayvanny, Mboso, Lavalava, Queen Darleen na wengine, ni bonge la bao kwa Kiba na Mofaya yake.

Pata picha Diamond anapanda jukwaani na MoFaya na kuwaambia mashabiki kuwa nishati yake ya kupiga shoo kali inatokana na kugida MoFaya. Hata sasa tu kitendo cha Kiba kuweka nia ya kudhamini Wasafi Festival kupitia MoFaya, na Diamond kuipokea nia hiyo kwa mikono miwili, jumlisha na jina la Kiba mwenyewe kama mmiliki, ni dhahiri kinywaji hicho kinasubiriwa chenyewe tu sokoni, kwani wateja wapo. Kuhusu mashabiki; Kiba na Diamond wakielewana na kusaini mkataba wa udhamini, kuna mashabiki wao watawakimbia. Ni wale ambao walikuwa wanapenda bifu lao kuliko muziki wao. Mashabiki matusi hawawezi kupenda maelewano hayo, maana watakosa fursa ya kuendelea kutukana.

Mashabiki waliompenda Diamond kwa sababu wanamchukia Kiba, na wenye kulazimisha mahaba kwa Kiba kisa hawamhusudu Diamond, hao wataondoka tu. Wao walitamani bifu liendelee. Mashabiki wa muziki wao na wenye kutamani mafanikio yao, wataendelea kuwaunga mkono. Watapata pia mashabiki wapya wanaopenda watu wenye akili. Diamond na Kiba wameonesha kupevuka kiakili.

Advertisement