Beka Flavour afunguka chanzo cha Yamoto Band kuvunjika

MIAKA miwili imepita tangu kuvunjika kwa kundi la Yamoto Band ambalo lilikuwa linabamba kinoma. Baada ya kufa kwa makundi ya Bongo Flava yaliyokuwa na mashabiki wengi kama East Coast, Wanaume Family, Wanaume TMK, Daz Nundaz vichwa vikakaa chini ya kuwakusanya vijana wanne wenye vipaji na kuunda Yamoto. Shukrani kwa Mkubwa Fela, ambaye aliwakusanya Beka Flavour, Aslay, Mbosso Khan na Enock Bella.

Baada ya kutamba sana, hatimaye Yamoto Band ikafa kifo cha kawaida bila kuibuka msuguano wala bifu miongoni mwa wasanii wake.

Hata hivyo, watu wakaanza kutengeneza mambo yao ili kuwaweka mbali wasanii hawa. Lakini, memba wa kundi hilo Beka Flavour amezungumza na Mwanaspoti kwenye mahojiano maalumu na kuweka wazi kwamba, bado wako karibu na wanawasiliana na kusaidia kwa hali na mali kama kawa.

Amesema kuwa wana kundi la mtandao wa kijamii wa ‘WhatsApp’, ambalo waliliunda tangu wako pamoja kikazi na mpaka sasa linaendelea kufanya kazi ya mawasiliano.

Pia, amefunguka mambo mbalimbali ikiwemo sababu za kuvunjika kundi hilo na ile mijengo yao waliyojengewa na Mkubwa Fella, ambaye ndiye alikuwa meneja.

Katika mahojiano yaliyochukua saa mbili, Becka alianza kwa kuelezea kidogo kuhusu Yamoto kwamba, lilianzishwa mwaka 2014 na baadaye kutamba na ngoma kali kama ‘Najuta’, ‘Niseme’, ‘Nitakupwelepweta’, ‘Cheza kwa Madoido’ na nyingine kibao na miaka mitatu baadaye yaani mwaka 2017, historia ikafika mwisho na kuvunjwa.

CHANZO YAMOTO KUVUNJIKA

Mengi yamesemwa kuhusu kuvunjika kwa Yamoto. Kila mtu alisema lake. Wapo waliodai kuwa wasanii wa kundi hilo waligombana wenyewe kwa wenyewe.

Wapo waliodai chanzo ni kuishiwa uwezo wa kutunga nyimbo na walikuwapo pia waliodai kwamba, Aslay alijiona analibeba kundi hivyo akaamua kujiweka pembeni ili afanye kazi zake.

“Hapa ukimya wetu ndio umezalisha mambo hayo... uvumi umekuwa mwingi sana kuhusu sababu za kuvunjika kwa Yamoto. Lakini, ukweli ni maslahi tu ndio chanzo cha kundi letu kusambaratika.
“Ninapozungumzia juu ya maslahi namaanisha hivi: Tulikuwa tukifanya shoo na kupata Sh10 milioni na kwenye bendi tuko wasanii watano, ambapo wanne waimba na mmoja dansa ambaye ni Chiba.

Nyuma yetu kuna watu kama saba hivi kwa maana ya wapiga vyombo kisha kuna Mkurugenzi Said Fella, Meneja Chambuso na Babu Tale alikuwepo. Pia, kuna mtayarishaji Shirko. Sasa unaweza kuona hayo malipo ya shoo yanakwenda kugawanywa vipi hapo ili mtu uweze kufanya maendeleo? Kuna wakati mgawo unakwenda hadi 50,000 kwa shoo.

“Hapo ndio waimbaji ambao Mimi, Aslay, Enock na Maromboso tukakutana na kujadiliana nini cha kufanya na kukubaliana kwamba, kila mmoja anaweza kusimama mwenyewe akaenda studio na kufanya kazi zake binafsi.

Baada ya kukubaliana tukaenda kwa Fella na kumueleza hilo na yeye akatoa ruhusa na kutupa baraka zake.

“Kila msanii akaanza kutoa ngoma zake na kupeana sapoti na hadi kila mmoja kasimama vizuri... Mbosso yuko na WCB, Enock Bella naye katoa ngoma zake kama mlivyozisikia na uzuri wa sisi kila moja ni mtunzi hatukuwa tunatungiwa na watu pembeni,” anasema Beka.

Hata hivyo, Beka anafunguka zaidi kwamba, Fela aliwahoji kama tatizo ni fedha basi wanapaswa kuwa na uvumilivu kwa kuwa fedha zinapatikana na ni suala la muda tu.

“Alitushauri kama mzazi wetu, lakini tukamwambia atuache kwanza tujaribu na kuona kama tumekomaa kimuziki bila ya kusimamiwa. Akasema basi ni sawa fanyeni kazi,” anaongeza Beka.


NYUMBA ZAO NA FELLA SASA
Kipindi Yamoto bendi inafanya kazi, Fella  alieleza kuwa ameamua kuhakikisha kila msanii wa Yamoto anakuwa na mjengo.

Akanunua viwanja na kuanzisha ujenzi huku akionyesha makazi hayo kwenye vyombo vya habari. Wapo ambao hawakuamini, lakini baadaye kila kitu kikawekwa wazi huko Kisewe. Lakini, baada ya kundi kuvunjika huko mitandaoni na mitaani kila mmoja anasema lake kuhusu mijengo hiyo. Hapa Beka anafunguka mpango mzima ulivyo:

“Hakuna aliyedhulumiwa nyumba,  na sio kitu rahisi kudhulumu, hivyo ni vitu tu vinatengenezwa kumchafua Fella. Nyumba tangu zimeanza kujengwa zinaonekana na hadi waandishi wa habari waliitwa sasa inakuwaje leo kuwe na mabadiliko kuhusu nyumba.
“Kila mtu ana nyumba yake pale na zimeshaisha bado vitu vidogo sana kukamilika na hapo kila mmoja anaweza kukamilisha mwenyewe na akiamua kuishi hapo sawa.

Mbosso amaeshavuta na umeme kwake na amemuweka mtu anaishi pale ila sisi wengine bado hatujaweka watu. “Narudia tena watu wafahamu Fella hahusiki tena na zile nyumba, na mwanzo zinajengwa tulikubaliana sisi wahusika, pesa itakayopatikana tusigawane tumkabidhi Fella akatusimamie ujenzi sababu sisi ilikuwa ni watu wa kusafiri sana, ikawa hatuwezi kupata pesa halafu tukasimamie ujenzi wakati hatupo Dar es Salaam.

“Lakini, tumeandikishiana na kila mmoja ameandika jina lake kwenye umiliki...,” anasema Beka.

HATAMANI KURUDI YAMOTO

Beka Flevor anasema hatamani kurudisha miaka nyuma kuwa Yamoto Band, kwa sababu angekuwa hapati kile anachotaka tangu ameanza kufanya kazi zake binfsi...hatamani kurejea huko.

“Baada ya bendi kuvunjika kila moja anaendesha maisha yake na nakwambia Yamoto Band ingekuwepo hadi leo, nahisi tungekuwa ‘levo’ nyingine.

“Tulikuwa na upepo wa kupendwa na tulikuwa na kichwa kizuri cha kutunga nyimbo za kuwateka mashabiki, yaani ningekuwa na uwezo ningeirudisha hiyo bendi tungefanya biashara kubwa kwa sababu kila mtu ameshatengeneza mashabiki nje ya kundi.

Kwa mfano tupige shoo kisha kila msanii avute mashabiki 1,000 hapo mnapiga pesa kwa kuwa, kila mmoja atakuja kumuona msanii wake,” anasema Beka.

KUNDI LA WHATSAPP

“Msanii zaidi ninayewasiliana naye sana katika kundi Enock Bella, Aslay nawasiliana naye ila sio sana na mara nyingi tumekuwa tukibanwa na majukumu...huwezi kuamini kuna wakati ananialika kwenye matukio yake lakini, nashindwa kutokea kwa sababu nakuwa nje ya mkoa.

Kwa upande wa Maromboso sijawasiliana naye muda mrefu sana niseme tu ukweli, sababu huenda ubize wa kila mmoja, lakini hadi leo hatujavunja group letu la Yamoto Band, hivyo mtu akitoa kazi yake anatupia humo na kunatoa maoni.”

BIFU NA ENOCK BELLA

Anasema Beka Flevor kuwa, alishawahi kugombana na Enock Bella na kununiana siku tatu wakiwa ziarani nchini Marekani.

“Yaani tulikuwa tumepangiwa hoteli chumba kimoja tulikuwa tunakaa watu wawili, nilikuwa nakaa na Enock, sasa akaja mtu kuniita alikuwa na shida na mimi, nikatoka nje namaliza kuzungumza na yule mtu nataka kuingia ndani Enock akafunga mlango na kushindwa kufungua.

Nikagonga sana lakini mlango haukufunguliwa na kama unavyojua lile baridi la Marekani...nikaganda sana hadi baadaye nikafanikiwa kuingia ndipo tuligombana sana tukanuniana siku tatu.

Lakini, siku zote sisi ni ndugu hivyo, tulikuja kupatana bila hata kupatanishwa na mtu na ukiangalia ile safari tulikwenda wenyewe bila Fella wala Chambuso. Walibaki nyumbani kwa sababu viza zao zilikuwa zimekwisha na huo ndio ugomvi mkubwa uliowahi kutokea kwangu na mwenzangu,” anafichua Beka.

Hata hivyo, Beka anaeleza kuwa mpaka sasa wanaendelea kumheshimu Fela kama mlezi kwani, amewaonyesha njia sahihi katika maisha na sasa wameweza kusimama wenyewe.

“Wakati natoka kwetu Ifakara ara hadi kufika Dar es Salaam nilikuwa naishi mwenyewe japo nina ndugu zangu na hadi kukutana na Fella na kuanza kuwa chini yake hvyo, sitamsahau kabisa katika maisha yangu na nitamheshimu sana.

KUMBE HAKUTAKA MUZIKI

Beka, ambaye ametamba na nyimbo kama Libebe, Kibenten, Sikinai, Siachani Naye, Sarafina na nyingine nyingi anafunguka kwamba, tangu ameondoka Yamoto Band maisha yake yamebadilika na kipato kimeongezeka kwa kasi.

Je unafahamu kitu gani kinaendelea sasa hivi kwa Beka...ishu ya familia yake imekaaje na kitu gani anatamani zaidi kwa sasa..Fuatilia kesho Jumatatu