Diamond atunukiwa tuzo Canada ya kutangaza Kiswahili

Muktasari:

Msanii wa muziki nchini Tanzania, Diamond Platnumz ametunikiwa tuzo ya kutangaza lugha ya Kiswahili kupitia muziki iliyotolewa na taasisi ya Swahili Vision International Association(SVIA).

Dar es Salaam. Siku chache baada ya kupata tuzo ya BOA, msanii wa Bongofleva nchini Tanzania, Diamond Platnumz amepata tuzo nyingine ya kutangaza Kiswahili.

Katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, Meneja wake Babu Tale ameweka picha ya tuzo hiyo, iliyotolewa na Swahili Vision International Association(SVIA).

SVIA ni umoja wa wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili wanaoishi nchini Canada ulioanzishwa kwa lengo la kuikuza na kuitangaza lugha hiyo.

Katika picha ya tuzo hiyo, Tale aliandika “Wakiona mbali inatosha, japokuwa nyumbani wanajitia upofu juu ya juhudi za kijana mwenye kukitangaza Kiswahili nje ya mipaka ya Tanzania. Pambana mwanangu Diamond sanamu lako litakaa hata sebuleni kwangu itatosha.”

Akizungumzia kauli hiyo Tale amesema anaziona juhudi za Diamond na amefurahishwa na wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili nje ya Tanzania kuziona juhudi zake.

“Furaha tu imezidi, hakuna jingine, ila natamani na wengine hususani hapa nchini wangeziona juhudi hizo,” amesema Tale.