KAJALA: KHA! Jamani ada mnalipa nyie!

Friday February 1 2019

 

By RHOBI CHACHA

KAMA kuna mzazi anayepitia kwenye wakati mgumu kwa sasa kutokana na matokeo ya kidato cha nne basi ni staa wa Bongo Movie, Kajala Masanja.

Huko kwenye mitandao ya kijamii watu hawalali na hawataki kuishiwa bando unaambiwa kisa, kufuatilia kila kinachoendelea na wiki iliyopita ishu iliyotrendi kinoma ni hayo matokeo ya kidato cha nne.

Ndio, si unafahamu kuwa mtoto wa Kajala, Paula ambaye amekuwa maarufu sana kwenye mitandao ya kijamii akifuata nyayo za mama yake, matokeo yake hayakuwa mazuri sana.

Japo wataalamu wanakwambia unaweza kuwa na akili nyingi lakini, kwenye mitihani ukaanguka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo hofu ama kutegemea siku hiyo ulikuwa kwenye hali gani.

Lakini, baada ya vichambo huko mitandaoni Kajala ameamua kufunguka akishangazwa na watu kufuatilia na kutokwa povu na matokeo ya mwanaye, Paula.

Pia, amewataka watumiaji hao wa mitandao kufahamu kwamba, Paula ana wazazi sio yatima na kusisitiza kuwa anamuachia Mungu kuwahukumu.

“Nafahamu kila kinachoendelea huko mtandaoni kuhusu matokeo ya Paula, niliamua kukaa kimya kwa kutojibizana na watu ili mwanangu abaki kuwa salama.

Watu wanatakiwa kufahamu kuwa Paula ana wazazi wake, sio yatima hivyo kamwe hatakuwa mpweke.

“Nashangazwa na inaumiza watu wanaacha kazi na kuanza kumrushia maneno makali mwanangu kwa lengo la kumkatisha tamaa, yaani kama ndio waliokuwa wakimlipia ada na huduma zingine. Watambue kuwa siwezi kumuacha mwanangu alie peke yake, nitakuwa naye kumtia moyo na kujipanga upya katika eleimu yake na atasoma hadi chuo kikuu,” amefunguka Kajala.

Pia, ameeleza kuwa matokeo ya Paula hayana maana kwamba, hakulelewa kwenye malezi sahihi na kumfanya kutumia muda mwingi kwenye mitandao na bata.

“Unajua jambo linapotokea basi utayasikia mengi sana, Paula sio mtu wa starehe ya kwenda klabu sasa wamemuona wapi? Au ni malezi gani wanayataka nimlee mwanangu kwa sababu namlea kwenye maadili mema au hawataki niwe karibu na mwanangu ama kuwa na akaunti ya instagramu ni nongwa?.

“Naomba wamuache mwanangu jamani, imetosha sasa na hao wanaotoa kauli za kejeli wenyewe wamesoma, narudia tena Paula atasoma hadi chuo kikuu na atakuja kuwashangaza,” alijimwaga Masanja.

Advertisement