Kusah afunguka Ruby kuimba kabla ya 40

Tuesday April 16 2019

 

Mzazi mwenzie msanii Ruby, Salmin Ismail anayejulikana kwa jina la kisanii ‘Kusah’, amesema kitendo cha mkewe kwenda kufanya shoo kabla ya kumaliza siku arobaini tangu ajifungue, hakukurupuka bali wamezingatia ushauri wa daktari.

Kusah ambaye pia ni mwandishi wa nyimbo na ndiye aliyemwandikia Ruby wimbo wa Ntade na Alele, alikiri awali kusikia maneno kuwa mzazi huweza kupata tatizo endapo hatamaliza arobaini.

“Kutokana na hilo kabla hajaanza kufanya shoo, ilitubidi twebnde tukapate ushauri wa daktari ambaye alitueleza kuwa hilo halina shida.

“Pia kama mmefanikiwa kumuona Ruby akienda kwenye shoo hakai zaidi ya saa, na sio kila shoo anaenda hivyo kama ni muda wa kukaa na mtoto anaupata,” alisema.

Akitolea mfano siku ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya shule za Kisarawe, alisema shoo hiyo ilitokana na ukaribu wake na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo.

Kwa upande wa shoo aliyoifanya kwenye shughuli ya utoaji tuzo ya Malkia wa nguvu, iliyofanyika Aprili 6, mwaka huu, alisema hakuna asiyejua Ruby kakulia kwenye familia ya kampuni ya Clouds.

Advertisement

Hata hivyo, alikanusha maneno ya watu wanaosema kwamba mzazi mwenzie huyo anafanya kazi kutokana na hali ngumu ya kifedha na kusema hata bila shoo wanaweza kuishi.

Kuhusu mtoto anasema wakati Ruby akienda kwenye shoo huwa anakuwa katika uangalizi makini wa bibi yake (mama wa Kusah) na kwamba yuko na Ruby tangu alipojifungua.

Akizungumzia mipango ya ndoa, alisema hivi karibuni watu watarajie lolote kutoka kwao kwa kuwa msanii huyo ni mtu mwenye malengo naye.

Advertisement