Man Water atamani bifu la Kiba, Diamond lidumu milele

Sunday December 30 2018

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mtayarishaji wa siku nyingi wa muziki, Man Water amesema anatamani bifu kati ya Ali Kiba ‘King Kiba’ na Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ liendelee milele.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumamosi Desemba 29, 2018, Man Water ambaye amewahi kutengeneza nyimbo mbalimbali za wawili hao kwa nyakati tofauti, amesema bifu lao ndilo linalosababisha muziki wa Bongo kuwa mtamu.

Amekwenda mbali zaidi na kueleza endapo wawili hao ikatokea siku wakapatana basi muziki wa Bongo utadorora.

“Yaani hawa wasanii wakipatana ni sawa na kutokuwepo kwa timu ya Simba na Yanga, hivyo waacheni waendelee hivi hivi jamani kwani ndio burudani yenyewe,” amesema.

Hata hivyo, mtayarishaji huyo alibainisha wasanii wote hao anawajua vilivyo na bifu walilonalo si wanalofikiria watu huko mtaani bali ni la kimuziki katika kuifanya biashara yao iendelee.

Advertisement