Mwana FA alivyofika kilele cha Mlima Kilimanjaro

Muktasari:

Kama unapitia mitandao mbalimbali ya kijamii kuanzia jana na leo Ijumaa Oktoba 4, 2019 lazima utakuwa umekutana na picha inayomuonyesha msanii wa Bongo Fleva, Mwana FA akiwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Dar es Salaam. Kama unapitia mitandao mbalimbali ya kijamii kuanzia jana na leo Ijumaa Oktoba 4, 2019 lazima utakuwa umekutana na picha inayomuonyesha msanii wa Bongo Fleva, Mwana FA akiwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Mwana FA alikuwa miongoni mwa wasanii waliopanda mlima huo ikiwa ni sehemu ya kampeni ya ‘Twenzetu kileleni’ iliyoratibiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii,  Dk Hamisi Kigwangalla.

Wakati wasanii wengine wakishindwa kufika kilele cha mlima huo, wengine wakishindwa kabisa kupanda kwa Mwana FA hali ilikuwa tofauti, alipanda na kufika kileleni.

Akizungumzia  hatua hiyo, amesema haikuwa rahisi na kwamba hakupanga kupanda mlima huo kw akuwa alikwenda mjini Moshi, Kilimanjaro katika uzinduzi wa kampeni hiyo tu.

“Nilikuja kuunga mkono kampeni na nilipanga kushiriki kwenye uzinduzi kisha nirudi, nilipofika hapa katika maongezi watu wakawa wananizingua kwamba siwezi kupanda.”

“Yani walikuwa wananiweka kundi moja na Steve Nyerere nikaona niwaonyeshe kama naweza nami nikawa miongoni mwa wanaopanda mlima na hatimaye nikafika kileleni,” amesema Mwana FA.

Ameongeza, “Kule kunaleta raha yaani ni adventure kwa kweli ingawa sio kazi rahisi unatembea na wakati mwingine hadi unatambaa kupanda mlima, unatafuta jiwe upumzike unakutana na jiwe la barafu inabidi ukae kisha uendelee na safari.”