Mzee Yusuf: Ujasiri wa Leyla umemnusuru na kipigo cha majambazi

Tuesday January 8 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Aliyekuwa mwimbaji taarabu, Mzee Yusuf amesema ujasiri wa mkewe, Leyla Rashid, umemsaidia kupambana na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi waliowavamia nyumbani kwao Chanika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi  leo Jumanne Mzee Yusuf ambaye sasa ni mwalimu wa dini amesema pamoja na majambazi hao kumuumiza mkewe ila naye aliwapa kipigo kidogo.

Akisimulia tukio lilivyokuwa, amesema ilikuwa ni majira ya saa 2:30 usiku jana Jumatatu wakiwa sebuleni wanaangalia TV, wakasikia kishindo cha watu kikitua ndani ya uzio wakajua wamevamiwa na wahalifu.

"Mimi kwa haraka nilipochungulia niliwaona wawili nje nikawafuata kupambana nao kumbe walikuwa zaidi ya saba na wawili walikuwa getini.”

"Huku nyuma watatu wakaingia ndani na kukutana na mke wangu huku wakimtaka awaonyeshe hela zilipo na kumtisha kwa bunduki, ingawa mke wangu haraka sana alibaini ilikuwa bunduki bandia ndipo alipoanza kupambana nao, ”anasema Yusuf.

Anasema kwenye mapambano hayo kwa sababu walikuwa wengi walimzidi nguvu na kumpiga mateke ya tumboni yaliyopelekea kusikia kizunguzungu na kuanguka.

“Baadhi yao tunawafahamu, wanaishi hapa mtaani na mara nyingi majirani wamekuwa wakiwahisi wana tabia hiyo ya wizi, ”anasema na kuongeza kuwa mbali ya kumjeruhi mkewe pia wamemjeruhi mtoto wake.

Alitaja vitu vilivyoibiwa mbali na fedha kuwa ni simu na  vifaa vya shule vya watoto.

“Mke wangu yupo hospitali akifanyiwa vipimo mbalimbali, amekuwa akilalamika kusikia vitu vinakata tumboni, ”anasema Yusuf.

Advertisement