Rapa ASAP Rocky wa Marekani aendelea kushikiliwa Sweden

Muktasari:

Rapa huyo alikamatwa baada ya kufanbya onyesho, akituhumiwa kumshambulia kijana mmoja mtaani akiwa na msafara wake.

Waendesha mashtaka wa Sweden wameomba rapa wa Marekani, ASAP Rocky aendelee kushikiliwa mahabusu wakihofia kuwa anaweza kuhusika tena katika mapigano baada ya kutokea vurugu jijini Stockholm, licha ya maombi kutoka kwa wasanii wenzake wakitaka aachiwe huru.
"Tumekuwa tukifanyia kazi sana uchunguzi na sasa tunahitaji hadi Alhamisi kukamilisha uchunguzi wa awali," alisema mwendesha mashtaka, Daniel Suneson, katika taarifa yake.
Mwimbaji huyo wa muziki wa rap mwenye umri wa miaka 30 na ambaye jina lake halisi ni Rakim Mayers, alikamatwa Julai 3 usiku wa maanani akiwa pamoja na watu wengine watatu kutokana na kupigana mtaani Juni 30. Mmoja wao, ambaye ni mlinzi wa Mayer, aliachiwa huru baadaye wiki hiyo.
Julai 5, Mahakama ya Wilaya ya Stockholm iliamuru kuwa Mayers ashikiliwe mahabusu wakati uchunguzi wa kesi yake ukiendelea kwa kuwa alikuwa akidhaniwa kuwa angeweza kutoroka Sweden.
Mahakama hiyo iliwapa waendesha mashtaka muda hadi Julai 19 kuamua kama watafungua mashtaka.
Kwa mujibu wa mahakama hiyo, usikilizaji mpya wa shauri la ASAP Rocky na watu wengine wawili walio mahabusu, utaanza baadaye Ijumaa.
Mamlaka ya Uendeshaji Mashtaka ya Sweden ilisema mwendesha mashtaka mpya, Daniel Suneson, amechukua jukumu la uchunguzi kutoka kwa Fredrik Karlsson kwa kuwa ilikuwa ni kipindi cha likizo.
Mwanasheria wa Mayers, Slobodan Jovicic aliliambia gazeti la Expressen wiki iliyopita kuwa jambo muhimu lililozingatiwa katika kuongeza muda wa kushikiliwa kwa mteja wake katika shauri jipya ilikuwa ni ama kupata ushahidi kwamba Mayers hakuwa anataka kutoroka au kujenga hoja kuwa haikuwa haki kumuweka mahabusu kama uchunguzi ungerefushwa.
"Mahakama ingeweka msimamo kuwa wiki mbili zinatosha, na si zaidi ya hapo," alisema Jovicic.
Rapa huyo amesema alikuwa akijihami baada ya kuchokozwa na vijana wawili ambao walimnyanyasa na kumfuata yeye na wenzake.
Sehemu ya tukio hilo ilinaswa na kamera ya video na kuchapishwa kwenye gazeti la watu maarufu la TMZ.
Katika video hiyo, rapa huyo, ambaye alikuwa Stockholm kutumbuiza kwenye tamasha, anaonekana akimrusha mmoja wa vijana hao mtaani na baadaye kumsukumia makonde wakati akiwa chini.
Mayers pia alituma mtandaoni video yake Julai 2 ambayo anasema inaonyesha hali ilivyokuwa kabla ya tukio hilo.
Katika video hiyo, viujana hao wawili wanaonekana wakibishana na mwanamuziki huyo kuhusu spika za masikioni na msanii huyo anawasihi waache kumfuata.
Mmoja wa vijana hao anaonekana akimpiga mmoja wa watu wamkiundi la rapa huyo.
Wasanii kadhaa wenzake kama Post Malone, Sean "Diddy" Combs, Nicki Minaj, Meek Mill na Justin Bieber wameandika katika akaunti zao za mitandao ya kijamii wakimuunga mkono rapa huyo.