Rapa Lizzo aongoza kuwania tuzo nyingi Grammy

Friday November 22 2019

 

Mwimbaji na rapa, Lizzo ndiye anayeng'ara kwenye orodha ya wasanii waliotajwa kuwania tuzo za muziki za Grammy 2020 akiwa ametajwa katika tuzo nane.
Lizzo anaongoza orodha iliyojaa wasanii wapya, kama Billie Eilish na Lil Nas X-- aliyeng'ara ndani ya muda mfupi-- katika kuwania tuzo kubwa za tamasha hilo.
Lizzo, 31, aliibuka mwaka 2013 lakini alianza kujulikana zaidi mwaka huu alipotoa albamu yake ya tatu ya "Cuz I Love You," ambayo imetangazwa kuwania tuzo ya Albamu ya Mwaka katika tamasha hilo litakalofanyika Januari 26 katika ukumbi wa Stapple Center.
Eilish pia ametangazwa kuwania tuzo ya albamu bora kutokana na kazi yake ya "When We All Fall Asleep, Where Do We Go?" na kufanya awe katika kinyang'anyiro cha tuzo sita, kama ilivyo kwa Lil Nas X ambaye alipata umaarufu kutokana na kazi yake ya "Old Town Road" na kujikuta akiwania tuzo sita.
Wanamuziki hao watakabiliana na upinzani kutoka kwa wasanii nyota.
Ariana Grande -- ambaye albamu yake ya "Thank U, Next" ilichelewa katika tuzo za mwaka jana -- mwaka huu ametajwa kuwania tuzo tano.
Naye Beyonce atakuwa katika kinyang'anyiro cha tuzo nne.

Advertisement