Rwanda yapinga uchunguzi huru kifo cha msanii wa muziki wa injili

Friday February 21 2020

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Rwanda. Rwanda imepinga shinikizo kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu yanayotaka ufanyike uchunguzi huru kuhusu kifo cha kifo cha msanii maarufu wa nyimbo za injili nchini humo, Kizito Mihigo.

Mihigo alikutwa amekufa kituo cha polisi Jumatatu ya Februari 17, 2020 karibu na mpaka wa Burundi, alikuwa akituhumiwa kwa jaribio la kutaka kutoroka nchini humo kwenda kujiunga na kundi la waasi linalopigana dhidi ya serikali ya Rwanda.

Mihigo aliyejizolea umaarufu kutokana na ujumbe wake wa amani na maridhiano alipigwa marufuku kuondoka nchini Rwanda kutokana na kukabiliwa na mashtaka.

Kutokana na utata wa kifo chake, ambacho Polisi walidai alijinyonga kwa nguo aliyokuwa akiitumia kulalia,  mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch, Amnesty International na Commonwealth Human Rights Initiative yamekuwa yakishinikiza kufanyika kwa uchunguzi huru wa kubaini mazingira yaliyosababisha kifo cha mwanamuziki huyo.

Hata hivyo, Serikali ya nchi hiyo imepinga jambo hilo ambapo msemaji wa shirika la upelelezi la Rwanda, Marie Michelle Umuhoza, ameliambia Shirika la Habari la BBC kuwa, “Rwanda ni nchi huru inayojitawala na ambayo ina uwezo wa kufanya uchunguzi  wa kitu chochote.”

Ofisa wa Human Rights Watch ameiambia BBC kwamba uchunguzi huru utaangalia kamera za siri katika eneo ambalo msanii huyo alikuwa anazuiliwa.

Advertisement

Umuhoza amesema Rwanda tayari inafanya uchunguzi kuhusu kifo chake.

Mihigo aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 mwaka 2015 kwa kupanga njama ya kupindua Serikali na baadaye kuachiwa kwa msamaha wa rais Septemba 15, 2018 pamoja na wafungwa wengine zaidi ya 2,000.

Advertisement