Simulizi za muziki: Katibu alipotoweka na fedha za kiingilio

Saturday November 9 2019Anko Kitime

Anko Kitime 

By Anko Kitime

Ni miaka zaidi ya 36 sasa toka nimejiunga na bendi ya kwanza ya muziki.

Katika miaka hii nimekutana na mambo mengi yaliyosababisha hisia mbalimbali kama furaha, machungu, maudhi na mshangao.

Leo najaribu kukumbuka baadhi ya matukio na vituko nilivyowahi kukumbana navyo.

Kwanza nianze na tukio lililonikuta siku ya mkesha wa Krisimasi mwaka 1976. Tukiwa na wenzangu na kabendi ketu kadogo pale Iringa tuliamua kwenda kupiga muziki katika kijiji cha Ilula Isele ili tupate fedha za kusherehekea sikukuu hiyo. Isele kulikuwa na ghala la mbolea lililokuwa tupu na tukawa tumepata ruksa na uongozi wa kijiji tulitumie.

Matayarisho yote yalienda sawa na mlangoni aliyekuwa akikusanya kiingilio alikuwa katibu wa bendi yetu. Watu walikuwa wengi na tulitegemea kupata fedha nyingi.

Dansi lilipoisha, hatukumuona katibu, alikuwa kapotelea gizani. Tukawa hatuna ujanja bali kulala mulemule ghalani mpaka kesho yake.

Advertisement

Tuliamka tukiwa hatuna chochote, saa sita mchana ilitukuta hatujanywa hata chai na hatukuwa na taarifa yoyote ya katibu wetu wala fedha. Baadaye tulikuja kupata taarifa kuwa alionekana akiondoka na akina dada wawili muda mfupi kabla ya dansi kwisha.

Tukaamua kupiga dansi la kuanzia saa 8 mchana mpaka saa 12 jioni, japo tupate nauli ya kurudi Iringa mjini. Mambo hayakuwa mabaya kufikia saa 12:00 jioni tulikuwa na fedha ya kutosha kununua chakula na kurudi nyumbani. Katibu alionekana baada ya wiki akidai kuwa alichukuliwa kiuchawi na watu asiowajua.

Kuna jambo ambalo nilishiriki mara mbili ambalo si rahisi kulisikia likifanyika japo ni zuri. Ilikuwa mwaka 1987, nilikuwa katika bendi tuliyoiita TX Seleleka, bendi hii ilikuwa ni ile ile ambayo hadithi yake nimewaeleza hapo juu.

Hakika tulikuwa tumepanda daraja maana tulifikia hatua ya kupata mkataba wa kupiga katika ukumbi wa Bandari Grill kwenye hoteli ya New Africa, jijini Dar es Salaam. Tulikuwa tumepitia safari ndefu toka kulala kwenye ghala tupu Ilula.

Baada ya mkataba wa New Africa kwisha tuliamua kuvunja bendi. Tulijipanga tukarudi Iringa na kufanya onyesho la mwisho la bendi katika ukumbi uliokuwa ukiitwa Bank Club kwa siku hizi ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki (Rucu). Baada ya onyesho hilo tuliendelea kula na kunywa mpaka asubuhi, ukawa ndio mwisho wa bendi. Wiki moja baada ya hapo nikajiunga na bendi ya Tancut Almasi Orchestra na kuwa mmoja wa waanzilishi wa bendi hiyo. Bado sijasikia bendi ikifanya ‘party’ ya kuvunja bendi.

Mwaka 1994 nilikuwa Vijana Jazz Band. Tulikuwa pamoja na mpiga gitaa mahiri Shaaban Yohana, ambaye alipewa jina la utani la Wanted na Hemed Maneti baada ya kutoka Tancut.

Kuna wanamuziki kadhaa ambao tulitolewa kutoka Tancut na Hemed Maneti katika kipindi hicho, alianza Shaaban Yohana akafuatiwa Mohamed Shaweji na Mohamed Gotagota, kisha nikaitwa mimi kujiunga na kundi hilo maarufu, hiyo ilikuwa mwaka 1989.

Mwaka 1994, mwanasiasa mmoja maarufu akaamua kuunda kundi la muziki jipya na Shaaban Yohana akaitwa huko. Shaabani akaitisha kikao cha bendi na kutueleza nia yake na kujiunga na kundi hilo jipya.

Hii ilikuwa si kawaida, mara nyingi mwanamuziki ulitoroka tu bila hata kuaga, lakini Shaaban aliitisha kikao ili kuaga na kuipa muda bendi kutafuta mpiga gitaa mwingine, ustaarabu huo ukawezesha Shakashia kujiunga na Vijana Jazz band akitokea MK Group, wakati Shaaban bado yuko na hivyo bendi iliendelea bila kupata athari kubwa.

Siku ya dansi la mwisho la Shaaban, tulimuaga vizuri na bendi ikamnunulia zawadi na akaondoka na kujiunga na bendi mpya ya Ngorongoro Heroes. Hili nalo si kawaida kuisha kwa furaha hivi.

Mwaka 1993, Vijana Jazz Band tulipewa kazi ya kuzunguka vijiji kadhaa huko Zanzibar kwenda kuhamasisha uvunaji bora wa karafuu.

Tulifika kupiga muziki katika kijiji kimoja, wakati tunaendelea kupiga muziki tukagundua mpiga gitaa mmoja ameanza kulewa lakini hakukuwa na kilevi chochote kinachouzwa pale.

Nilikuwa na wadhifa wa ‘stage master’, hivyo nikalazimika kutafuta pombe inatoka wapi.

Haikuchukua muda nikagundua kuna ofisa mmoja mpenzi mkubwa wa muziki alikuwa kaingia na chupa zake za pombe kali na ndizo alikuwa akiwagawia wanamuziki. Sikumchelewesha nikamfokea kuwa anachofanya kitasababisha muziki uharibike kabisa.

Na haikuchukua muda mrefu mwenzetu pombe zikamzidia akawa anatuharibia muziki, tulimzuia kupiga ili apumzike labda pombe zingempungua, lakini pombe zake zilimfanya alete fujo kubwa usiku ule hata baada ya onyesho, ikalazimika kesho yake asimamishwe kazi na kurudishwa Dar es Salaam.

Jambo la ajabu miaka kadhaa baadaye yule ofisa aliyekuwa anagawa pombe kwa wanamuziki alikuja kuanzisha bendi yake ambayo ilikuja kuwa maarufu hapa nchini.

Nilicheka sana siku nilipomkuta akilalamika kuwa kuna wapenzi wa muziki wanamharibia bendi kwa kuwalewesha wanamuziki wake na kuharibu nidhamu ya bendi nzima.

Advertisement