Wanamuziki kutumika kama mabalozi kwamkuna Msanii Vanessa Mdee

Muktasari:

Msanii wa Bongo Fleva nchini Tanzania, Vanesa Mdee amesema wasanii kutumika kuwa mabalozi wa huduma na bidhaa mbalimbali kunakuza muziki wa Tanzania.

Dar es Salaam. Mkali wa wimbo wa 'Bado', Vanessa Mdee amesema wasanii kutumika kuwa mabalozi wa huduma na bidhaa mbalimbali kunakuza muziki wa Tanzania.

Ameyasema hayo leo Ijumaa Februari 7, 2020, alipokuwa akitangazwa kuwa balozi wa sabuni ya Doffi inayozalishwa na kampuni ya Keds.

Msanii huyo amesema ubalozi ni jambo zuri kwa msanii ukizingatia bidhaa wanazozitangaza zinauzwa katika nchi mbalimbali.

“"Hii sabuni niliyochaguliwa kuwa balozi wake haiiuzwi tu hapa nchini kwani kampuni inayoitengeza ipo na nchi nyingine za Afrika.

“Hivyo kuonekana kwangu katika matangazo yao ni wazi kwamba na Mimi natumia kama jukwaa la kutangaza kazi zangu za muziki.

“Pia hii inaonyesha namna gani wasanii tunathaminiwa na wawekezaji hapa nchini, kwani wangeweza kumtumia mtu mwingine au hata vikaragosi ilimradi kuwafikia wateja wao lakini wameamua kufanya kwetu ambayo mbali ya kuwatangazia pia na Mimi naingiza fedha pamoja na nchi kwa ujumla kupitia kodi mbalimbali,” amesema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Koddes, Ben Song amesema wamemtumia Vanesa kwa kuwa ni msanii anayejituma na anatambulika nchi mbalimbali huku baadhi ya vijana hususan wasichana wakitaka kufikia mafanikio aliyo nayo

Song amesema wanaamini kwa nafasi aliyonayo msanii huyo, watawafikia wateja wao kirahisi.

Wakati kuhusu sabuni yao hiyo, amesema ni mwendelezo wa kampuni hiyo kuwekeza nchini ambapo mpaka sasa kutokana na uzalishaji wa bidhaa zingine zikiwemo taulo za watoto na wanawake, wametoa ajira za moja kwa moja 600 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 1000