#WC2018: Keisuke Honda na nahodha Hasebe wametundika daluga

Muktasari:
- Nyota wa timu ya taifa ya Japan, Keisuke Honda na mwenzake Makoto Hasebe wametangaza kustaafu soka la kimataifa, baada ya kushindwa kuivusha Japan katika hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Dunia, iliyoingia robo fainali jana.
Moscow, Russia. Nyota wa timu ya taifa ya Japan, Keisuke Honda na mwenzake Makoto Hasebe wametangaza kustaafu soka la kimataifa, baada ya kushindwa kuivusha Japan katika hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Dunia, iliyoingia robo fainali jana.
Wanasoka hao wamefikia uamuzi huo, baada ya Samurai Blues, kulimwa 3-2 na Ubelgiji, katika mchezo mkali wa mtoano, uliopigwa juzi usiku, katika Uwanja wa Rostov Arena mbele ya watazamaji 41,466, licha ya kuongoza 2-0, kwa mabao ya haraka yaliyopatikana kunako dakika ya 48 na 52, kupitia kwa Hataguchi na Takashi Inui.
Ubelgiji walifanya mabadiliko ya faida katika dakika ya 65, kwa kuwaingiza Nacer Chadli na Marouane Fellaini kuchukua nafasi ya Yannick Carrasco na Dries Mertens. Dakika nne baadae, Jan Vertonghen akafunga bao la kwanza, kwa kichwa safi.
Baada ya hapo, wakiongozwa na kiungo teleza, nahodha Eden Hazard, Ubelgiji walifanya mashambulizi mfulululizo katika lango la Japan ambapo katika dakika ya 74, Marouane Fellaini aliwasawazishia mashetani hao wekundu, kabla Nacer Chadli hajawafukia Japan katika kaburi la sahau katika dakika ya 90.
Honda ambaye ameifungia Japan mabao 37 katika michezo 98, hakuanza mchezo hata mmoja huko Russia, ambapo katika mechi ya juzi aliingia katika kipindi cha pili, huku mwenzake Hasebe ambaye alikuwa nahodha wa wajapani hao, alicheza mechi zote lakini walishindwa kuisaidia Samurai Blues.
"Ninaondoka nikiwa na furaha sana, tuna vijana wadogo wenye uwezo mkubwa wa kutufikisha mbali, lakini itoshe kusema tu kuwa hii ndio michuano yangu ya mwisho ya Kombe la Dunia kuvaa jezi ya Samurai Blue, kwa kawaida Samurai huwa hatukimbii mapambano ila kwa sasa inatosha," alisema Honda.
Kwa upande nahodha Hasebe, ambaye ameichezea Japan mara 114, alisema ana imani Japan itaendelea na moyo wa kupambana hata baada ya kung'olewa kwenye Kombe la Dunia na kuongeza kuwa kwa sasa anataka kuelekeza nguvu katika klabu yake ya Eintracht Frankfurt.
"Napenda kuchukua fursa hii, kuwashukuru mashabiki wa Japan kwa kutuamini na kutukabidhi jukumu la kubeba bendera ya taifa, tunajua hatukufanya mlichotarajia tukifanye na kwa hilo tunaomba radhi sana. Ahsanteni na kwaherini sana," alisema Hasebe.