Breaking News

UCHAMBUZI: Nani ana jukumu kuondoa uhaba wa vyoo shuleni?

Wednesday July 3 2019

 

By Edna Sonda

Umuhimu wa choo kwa maisha ya binadamu na katika kutunza usafi wa mwili na mazingira, unatambulika na kila mtu.

Inasikitisha na ni kero kubwa unapofika mahali kusipokuwa kabisa na huduma ya choo.

Shule ya Msingi Isike iliyopo katika Manispaa ya Tabora mkoani Tabora, ni moja ya shule zinazokabiliwa na kero hii.

Shule hii ina uhaba mkubwa wa huduma hii muhimu kwa maisha ya kila binadamu.

Ni jambo la kustaajabisha kuwa shule hii yenye jumla ya wanafunzi 1,221 ina matundu sita tu ya choo!

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa mwongozo kuhusu utaratibu wa vyoo shuleni.

Advertisement

Kwa mujibu wa mwongozo huu, tundu moja la choo linatakiwa lihudumie watoto wa kiume 25 tu.

Kwa upande wa wasichana, tundu moja linapaswa lihudumie watoto wasiozidi 20 tu.

Hii ina maana kuwa wavulana 611 walioko shule hii wanastahili kutumia matundu takribani 25, na siyo matatu wanayolazimika kubanana na kuyatumia kwa sasa.

Hali ni mbaya zaidi kwa wasichana; kwani wanalazimika kutumia mashimo matatu tu badala ya mashimo 30 wanayostahili kuwa nayo.

Hii ina maana kuwa katika shule hii wasichana wana upungufu wa matundu ya choo 27!

Ni wazi kuwa uhaba huu mkubwa wa matundu ya choo unawaweka wanafunzi katika hatari ya kupata magonjwa kama yale ya njia ya mkojo, kuhara, minyoo na hata magojwa ya mlipuko.

Lakini mtoto wa kike huwa katika hatari kubwa zaidi ya maambukizi na hutaabika kujistiri wakati wa hedhi kutokana na maumbile yake..

Changamoto haipo katika shule ya Isike pekee. Shule ya Msingi Gongoni nayo pia ina upungufu mkubwa wa matundu ya choo kiasi kwamba walimu wa jinsi zote hulazimika kutumia tundu moja la choo.

Hili ni jambo la kusikitisha. Upungufu mkubwa wa vyoo unazikumba shule nyingi nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu siku ya matumizi ya choo duniani mwaka 2017, kati ya shule za msingi 16,088 zilizoko nchini, zenye vyoo bora ni asilimia 28 tu.

Pia, kitabu cha Basic Education Statistics for Tanzania (Best) cha 2018 kinaonyesha kuwa hali ni mbaya katika shule nyingi za msingi za Serikali.

Takwimu zinaonyesha uwiano wa 1:58 badala ya 1:25 kwa wavulana na 1:55 badala ya 1:20 kwa wasichana.

Ukosefu wa huduma bora za vyoo ni moja ya sababu zinazochangia mahudhurio hafifu ya mtoto wa kike darasani. Aidha, takwimu hizo zinabainisha wasichana hawahudhurii shuleni kati ya siku nne hadi tano kila mwezi.

Vyoo visivyofaa kwa matumizi hasa kwa wasichana wanaoingia hedhi huleta changamoto kubwa kwao. Hivyo, huduma ya choo iende sambamba na upatikanaji wa maji shuleni.

Mwanafunzi anawezaje kujisafisha ikiwa shule haina maji hata kama kuna choo?

Tunapojisafisha, tunaondoa uwezekano wa kudhurika na magonjwa mbalimbali.

Katika maadhimisho hayo ya siku ya choo, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassani alisema:

‘’Endapo watoto wataendelea kuishi kwenye mazingira machafu na hatarishi, kuna uwezekano wa kuwa na watoto waliodumaa kimwili na kiakili.”

Serikali, mashirika na wadau wengine inatupasa tusaidiane kuongeza na pia kuboresha mazingira ya shule ikiwamo miundombinu kama vile idadi ya matundu ya vyoo, madawati, vyumba vya madarasa, maktaba, maabara na mengineyo katika shule zinazotuzunguka.

Vilevile viongozi wa ngazi zote wakati wanashughulikia suala la usafi wa mazingira na huduma ya choo bora, pia liende sambamba na ujenzi wa vyoo shuleni na upatikanaji wa maji safi na salama.

Wanajamii kwa ujumla inatupasa tusaidiane kuboresha mazingira ya shule zetu; tusisubiri kila kitu lazima Serikali ifanye. Hili la vyoo pia ni jukumu letu. Tuamke na tuanze kurekebisha baadhi ya mambo yenye upungufu katika shule zetu ili hata Serikali ikiona juhudi zetu, iwe tayari kuingilia kati na kutoa msaada mkubwa zaidi.

Katika zama tulizomo sasa, kama Taifa hatupaswi kabisa kufikiria masuala ya ujenzi wa vyoo kwa wanafunzi shuleni. Huko tulipaswa kutoka siku nyingi.

Sasa ni wakati wa kufikiria mambo makubwa zaidi kwa watoto wetu na sio vyoo kama tunavyoona sasa.

Edna Sonda ni mdau wa elimu. Anapatikanakupitia: [email protected]