Siku 100 bila Azory wala taarifa za uchunguzi

Muktasari:

Desemba 7, 2017 MCL, ilitoa taarifa ya kutoweka kwake kwenye vyombo vya habari, Jeshi la Polisi, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Spika wa Bunge, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na wadau wengine, kuomba msaada zisaidie kupatikana kwake.

Jana mwandishi wa habari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL, Azory Gwanda alitimiza siku 100 tangu alipotoweka katika mazingira ya kutatanisha Novemba 21, 2017 huko Kibiti, Mkoa wa Pwani.

Desemba 7, 2017 MCL, ilitoa taarifa ya kutoweka kwake kwenye vyombo vya habari, Jeshi la Polisi, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Spika wa Bunge, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na wadau wengine, kuomba msaada zisaidie kupatikana kwake.

Pia, MCL imepiga kampeni ya kumtangaza Azory kwenye kurasa za mbele za magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti na mitandao yake kwa kipindi chote hiki. Yote hiyo imefanyika kwa lengo la kusaidia kupaza sauti ili kila mwenye taarifa za mahali alipopelekwa mwananchi huyo atoe taarifa kwa vyombo vya dola.

Lakini, licha ya juhudi zote hizo, hadi wakati huu zinatimia siku 100 hakuna taarifa zozote kutoka chombo chochote iliyokwisha kutolewa kuhusu mahali Azory alipo. Pamoja na ukimya huo, bado tuna imani kwamba Azory atapatikana akiwa mzima na mwenye afya njema.

Tunaendelea kuviomba vyombo vyetu vya ulinzi na usalama wasaidie kupata jawabu la kitendawili hiki wao, hususan polisi ndiyo wenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao. Tunarudia kusema, kama kuna kosa lolote alilotenda, basi waliomkamata badala ya kumshikilia wamfikishe kwenye vyombo vya sheria ili haki itendeke.

Kitendo hiki kilichofanywa dhidi ya Azory ni cha uvunjaji wa haki za binadamu na ni kibaya kinachostahili kukemewa na kudhibitiwa haraka ndani ya nchi yetu ambayo ni kioo cha amani, upendo na mshikamano na ni mfano wa kuigwa na majirani zetu na hata nchi nyingine nyingi duniani.

Tunaomba tena, Azory arudishwe akiwa mzima na mwenye afya njema ili aungane na familia yake na wanahabari wenzake katika malezi na ujenzi wa Taifa letu kwa ujumla.

MCL bado ina imani kubwa na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Tunaamini kwamba vinaendelea kufuatilia mahali mwanahabari huyu alipo kama vilivyoahidi. Katika hili tunaungana na Inspketa Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kuwataka wale wote wenye taarifa za mahali Azory alipo wazifikishe kwenye chombo hicho na kama alivyoahidi, taarifa hiyo itakuwa siri.

Tunajua Watanzania wengi wako katika hali ya kufadhaika kuhusiana na matukio ya watu kutekwa na wengine kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Ili kuhakikisha hayo yanamalizika, tunatoa wito kwa Watanzania kutoa ushirikiano kwa jeshi letu la polisi kwa kutoa taarifa sahihi kuhusiana na watu wenye mwelekeo unaotia shaka kwenye jamii.

Usalama wa nchi yetu unajengwa na sisi sote, polisi hawawezi kuwapo katika kila kona ya nchi saa zote hivyo ni wajibu wa raia kutoa taarifa ikiwa wataona kuwapo kwa viashiria vyenye mwenendo wa uvunjaji wa amani.

Kila mmoja wetu akitimiza wajibu huu, kazi ya Jeshi la Polisi kupambana na wahalifu hawa waliopewa jina la ‘watu wasiojulikana’ itakuwa nyepesi. Sambamba na wito huo kwa wananchi, tunaliomba jeshi la polisi kuongeza kasi ya uchunguzi kuhusu mwanahabari huyo.