Tatizo ni mifumo ya kitaasisi au hatumuelewi rais

Miaka minne na ushee ya Rais John Magufuli bado inaonekana watumishi wengi wa umma hawajamwelewa Rais na pengine ndiyo maana hadi leo tunashuhudia kutenguliwa kwa teuzi mbalimbali.

Lakini si hilo tu, hadi leo hii bado tunashuhudia watumishi wa umma na hata wafanyabiashara wakiendelea kushitakiwa kwa ufisadi, jambo ambalo sasa tunapaswa kujiuliza tatizo ni nini?

Kabla na baada ya kuingia madarakani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Rais Magufuli alijipambanua kupambana na ufisadi na hili lilikuwamo pia kwenye ilani ya CCM 2015-2020.

Mojawapo ya mambo aliyoyaahidi Rais Magufuli ni kupambana na ufisadi na katika ukurasa wa 190 wa ilani hiyo, CCM iliahidi kuanzisha mahakama maalumu ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi.

Hii peke yake ilitakiwa itoe ishara kuwa Rais ajaye alikuwa hataki mchezo na hili limejidhihirisha kutokana na kauli na matendo yake kwa namna anavyoongea kwa hisia akionyesha kuchukizwa na ufisadi.

Wako ambao wanamkosoa, kwamba pengine vita yake dhidi ya rushwa inalenga kundi fulani la watu hasa wakosoaji wake wa kisiasa, lakini yapo mapapa ambayo bado yanakula kuku kwa mrija.

Bahati mbaya wengine ni makada wa chama chake na hili limethibitishwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole aliyetaka waumbuliwe kabla ya uchaguzi mkuu.

Polepole amenukuliwa katika video inayosambaa mitandaoni akitaka CCM itoe majina mapema ya mafisadi ili washughulike nao na wasisubiri kipindi cha uchaguzi Oktoba 2020.

“Kitu ambacho naweza kuikosoa CCM ni kuchelewa kuwatamka wezi, tunasubiri uchaguzi mkuu. Kama mnawajua mafisadi, wezi mtupatie majina tuanze kushughulika nao,” alisema Polepole.

“Tushughulike nao mapema ili tukifika wakati wa uchaguzi tusihangaike nao tena. Wako watu ndani ya CCM wanaonekana wa maana lakini hakuna kitu. Mimi najua nimekuwepo huko.

“Naomba kibali sasa tushughulike nao mapema ili tuuambie umma ‘msimwamini huyu si lolote si chochote, ni mwizi. Ndio, alikuwa na nafasi CCM ila ni mwizi’,” alisema Polepole.

“Kama kuna viongozi watovu wa nidhamu tuambieni. Wanaoweza kushambulia watu kwa hoja na maneno ni vijana na si watu wengine. Mtupe orodha mapema msichelewe,” alisisitiza Polepole. Polepole alitolea mfano wa ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika bandari ya Dar es Salaam mwaka 2016 ambapo alipewa orodha ndefu ya watu waliokuwa wamekwepa kodi.

“Mtu mmoja wa CCM alikuwa na kontena 700 hajalipa kodi. Sasa huyo si wamtaje tu wanachelewa nini. Mimi nitaenda kumuomba Mangula (Phillip) si mumtaje?” alihoji Polepole.

Ikiwa Rais ni mkali kama pilipili katika masuala ya rushwa na ufisadi si ndani tu ya Serikali, bali hata ndani ya chama chake ni lazima tujiulize tatizo liko wapi? Na ukali wote huu watu wanapiga dili?

Hili linaweza kuwa na majibu mengi, lakini tupende tusipende tunahitaji taasisi imara yenye mifumo imara katika kukabiliana na ufisadi kama alivyowahi kusema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyemaliza muda wake, Profesa Mussa Assad.

Inawezekana suala la kuendelea kwa ufisadi, utakatishaji fedha, uhujumu uchumi, ubadhirifu na wizi wa fedha za umma pengine unachangiwa na mfumo dhaifu tulionao.

Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia amewahi kusema yanayojitokeza katika utendaji wa Serikali hadi madudu yaendelee licha ya ukali wa Rais ni kukosekana kwa taasisi imara. “Lengo namba 16 la malengo endelevu ya dunia ni taasisi imara. Hii ni pamoja na katiba na sheria zetu. Hii ingewasaidia watendaji kujua majukumu yao,” alisema Mbatia.

Sasa mimi natamani rais angeona umuhimu wa kurejea mchakato wa kutunga kwa Katiba mpya iliyotokana na maoni ya wananchi, kwani hii ndilo suluhisho la hali tunayoishuhudia.

Rais angeacha jambo linaloishi (legacy) kama ambavyo alitamani kufanya Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, endapo katika kipindi cha uongozi wake, angetuachia Katiba mpya kama maoni yaliyopatikana katika Tume ya Jaji Warioba.

Kila mmoja leo anafahamu uzuri wa rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ilivyoziba kila mianya na kutengeneza mifumo imara ya kitaasisi katika kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania.

Ndiyo, Rais amekwisha sema katiba mpya si kipaumbele chake, lakini ukweli ni kuwa bila Katiba mpya itakayojenga uwepo wa taasisi imara, wallahi ataendelea kuteua na kutumbua hadi mwisho wa uongozi wake.