UCHAMBUZI: Yanga, klabu zijifunze kitu kupitia Zahera

Monday November 11 2019

 

By CHARLES ABEL

Baada ya kutimuliwa na Yanga, kocha Mwinyi Zahera amekuwa akianika masuala mbalimbali yanayohusu waajiri wake wa zamani katika mahojiano na vyombo vya habari.

Amekuwa akishambulia mashabiki, viongozi na hata wachezaji wa klabu hiyo kwa madai mbalimbali akiwaona kama ndio wamekuwa chanzo cha yeye kukutana na fyekeo ambalo limemtoa ndani ya Yanga.

Miongoni mwa tuhuma ambazo amekuwa akizitoa ni uongozi wa timu hiyo kumuingilia katika majukumu yake kwa kusajili baadhi ya wachezaji ambao hakuwa amewapendekeza na pia katika masuala ya kiufundi, kushindwa kuihudumia timu na pia kutokuwa na ushirikiano kwa benchi la ufundi na timu kiujumla.

Kana kwamba haitoshi, kocha huyo alienda mbali zaidi kwa kudai kuwa ameisaidia Yanga kiasi kikubwa cha fedha katika masuala mbalimbali kutokana na klabu hiyo kutokuwa vizuri kiuchumi.

Hata hivyo, uongozi wa Yanga haujajitokeza kujibu tuhuma hizo ila umeonyesha kutofurahishwa nazo kwa kuhisi kwamba kwa namna moja au nyingine zinaweza kuharibu sifa za klabu hiyo na pia kusababisha mgawanyiko na migogoro kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wake.

Tuhuma hizo ziwe za ukweli au za uongo, kuna darasa ambalo Yanga na timu nyingine hapa nchini zinapaswa kujifunza ili yasije kutokea tena na kuharibu taswira au nembo ya klabu husika kama ambavyo inatokea sasa kwa Zahera.

Advertisement

Jambo la kwanza ambalo Yanga na timu nyingine zinapaswa kujifunza ni kuweka vipengele vya kimkataba vinavyowabana waajiriwa wao kuzungumzia masuala yanayohusu klabu.

Hiyo itasaidia kuziweka klabu katika mazingira salama kwa kuwa hakuna mwajiriwa ambaye atakuwa tayari kukutana na adhabu ya kifungo au faini ya fedha hivyo atalazimika kuepuka kuzungumza masuala yanayohusu mwajiri wake.

Jambo la pili ambalo klabu zetu zinapaswa kujifunza kupitia sakata la Zahera ni kutoruhusu waajiriwa wao kuingilia au kufanya majukumu ambayo hayawahusu.

Zahera amefahamu mengi yanayoendelea ndani ya Yanga hata yale ambayo yalikuwa nje ya majukumu yake kwa sababu alikuwa anashirikishwa katika kila jambo linaloihusu klabu na laiti hilo lisingefanyika pengine leo hii asingekuwa na jeuri ya kuianika Yanga.

Kila mmoja ndani ya klabu anapaswa kufanya majukumu yake kama mkataba unavyoeleza badala ya kuingilia mambo yasiyomhusu kwani pia inaweza kusababisha mpasuko baina ya watumishi wa klabu. Zahera amedai kuna wakati alikuwa analipa posho wachezaji, gharama za kambi na mapungufu mengine.

Na kingine ambacho tunajifunza kupitia Zahera ni klabu zetu kujenga utamaduni wa kuonya na kuwachukulia hatua waajiriwa wao pale wanapofanya mambo kinyume na majukumu yao au wanapokosea.

Ni ukweli ulio wazi kwamba Yanga ilimlea Zahera na kumruhusu afanye mambo yasiyo ya weledi na badala ya kumuonya ilitumia nguvu kubwa kumtetea pasipo kujua kuwa inatengeneza mazingira ya kumfanya ajione Mfalme ndani ya klabu hiyo.

Mfano alipoadhibiwa kwa kuvunja kanuni ya masuala ya mavazi katika Ligi Kuu, uongozi wa Yanga ulitamka hadharani kuwa uko upande wa kocha wao na ukawatangazia wanachama, wapenzi na mashabiki wao kuwa wavae mavazi ya aina ileile ambayo yalisababisha Zahera achukuliwe hatua, kama ishara ya kumuunga mkono.

Lakini kama isingesimama upande wake na ingeonyesha kusikitishwa na kile alichokifanya, Zahera angejifunza kitu na kujiona kuwa hana nguvu kubwa ndani ya Yanga na hata katika mpira wa miguu hapa Tanzania.

Kingine ambacho ni darasa kutokana na kile kinachofanywa na kocha huyo wa zamani wa Yanga ni viongozi kuhakikisha timu zao zinakuwa na hali nzuri kiuchumi ambao utazifanya ziwe zinapata huduma nzuri na kwa wakati.

Ni aibu kiongozi wa klabu kuomba au kukopa fedha kwa kocha au hata mchezaji wakati yeye ndiye bosi na anapaswa kutazamwa pindi watu wa chini yake wanapokuwa na matatizo ya fedha.

Kitendo cha kutegemea fedha zitoke kwa kocha kinaashiria kwamba viongozi walishindwa kutimiza majukumu yao.