Chadema wapitisha wagombea watano wa udiwani Manyara

Muktasari:

Akizungumza na Mwananchi katibu wa chama hicho Mkoa wa Manyara, Gervas Sulle alisema chama hicho kimejipanga kushinda uchaguzi wa kata hizo.

Babati. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Manyara kimewapitisha wagombea watano wa udiwani watakaopeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika Agosti 12, mwaka huu.

Akizungumza na Mwananchi katibu wa chama hicho Mkoa wa Manyara, Gervas Sulle alisema chama hicho kimejipanga kushinda uchaguzi wa kata hizo.

Alisema chama hicho kitamsimamisha Mathias Zebedayo kugombea udiwani Kata ya Bagara mjini Babati.

Wagombea wengine ni Theophil Lolo wa Kata ya Masakta, Philipo Mallo (Gehandu), Zacharia Nihhi Tumati na Daniel Boa, Hayderer.

Alisema chama hicho kimejipanga kushinda kata hizo kwa kufanya kampeni za kistaarabu kwa kuuza hoja zao na kwamba endapo uchaguzi utakuwa wa huru na wa haki, wataibuka na ushindi.

“Kwenye kata nne kati ya tano, Chadema ilikuwa inaongoza udiwani, tunatarajia wananchi wa Manyara watawachagua tena wagombea wetu na kushinda upya uchaguzi huo mapema sana,” alisema Sulle.

Mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul alisema wananchi ndiyo watakaoamua kwa ridhaa yao kwa kumchagua mgombea udiwani mwenye uwezo wa kutetea masilahi yao.

“Chadema kwenye mikutano yetu ya ndani tumepanga mikakati; kesho (leo) tutaanza kampeni ya kumnadi mgombea udiwani Kata ya Bagara Mjini Babati, kwani awali ilikuwa kata yetu,” alisema Gekul.

Uchaguzi katika kata hizo unafanyika kufuatia madiwani wanne wa Chadema na mmoja wa ACT-Wazalendo kujiuzulu na kuhamia CCM kwa maelezo kuwa wanaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.

Katika mchakato wa kura ya maoni ndani ya chama hicho tawala, CCM imewapitisha tena wagombea hao waliokuwa madiwani wa Chadema na ACT, kuwania udiwani.

Uchaguzi wa kata 79 na Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma umepangwa kufanyika Agosti 12.