Maiti iliyogomewa kuzikwa Mbeya yafikisha siku ya 157 mochwari

What you need to know:

  • Frank alifariki dunia Juni 4 katika tukio ambalo liligubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai kijana wao ambaye alikuwa mfanyabiashara wa nguo za mitumba Soko la Sido jijini Mbeya, alifariki dunia kwa kipigo akiwa mikononi mwa Polisi, hivyo kususia mwili huo ambao hadi sasa upo chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo ikiwa ni siku ya 157.

Mbeya. Wakati mwili wa Frank Kapange ukifikisha siku ya 157 katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, gharama ya kuhifadhia mwili huo hospitalini hapo imefikia Sh3,140,000.

Frank alifariki dunia Juni 4, huku kifo chake kikigubikwa na utata uliodaiwa kutokana na mazingira ambayo ndugu hawakubaliani nayo.

Ndugu hao wanadai alikuwa mfanyabiashara wa nguo za mitumba soko la Sido na kwamba alikufa kutokana na kipigo alichopata akiwa mikononi mwa polisi jijini Mbeya.

Ndugu waligoma kuchukua mwili wake kwenda kuuzika wakisubiri hadi hatima ya rufaa waliyoiwasilisha Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya isikilizwe.

Ndugu wa familia hiyo chini ya wakili wao, Moris Mwamwenda waliliambia Mwananchi juzi kuwa wanasubiri hatima ya rufaa yao wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya iliyotupilia mbali maombi waliyoyawasilisha wakiiomba kutoa amri ya kufanyika uchunguzi wa kina juu ya sababu za kifo cha ndugu yao.

Agosti 24, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite aliamuru mwili wa Frank uchukuliwe na ndugu ili wauzike, baada ya kutupilia mbali maombi ya familia ya kuiomba mahakama hiyo iamuru kufanyika kwa uchunguzi wa kiini cha kifo chake, baada ya kuridhika na mapingamizi yaliyowasilishwa na mawikili wa upande wa Serikali.

Hata hivyo, ndugu hao walidai kutoridhika na uamuzi huo, hivyo walikata rufaa Mahakama Kuu.

Muuguzi mkuu wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Petro Seme alipozungumza na Mwananchi alisema bado wanaendelea kuuhifadhi mwili huo hadi watakapopokea amri nyingine kutoka mahakamani.

Seme pia alitaja gharama za kuhifadhi maiti hospitalini hapo kuwa ni Sh20,000 kwa siku moja.

“Sisi hatuwezi kufanya vinginevyo kwa sababu kazi yetu ni kuhifadhi maiti na hili suala la gharama nani atalipa tunasubiri hiyo amri ya mahakama,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Baada ya kujulikana hatima yake, ndipo tutakaa na wahusika ili kujua namna ya kulipa gharama hizo.”

Watawanyika nyumbani

Mlezi wa familia hiyo, Julius Kapange alisema baada ya ndugu kufanya mazungumzo na wakili wao Mwamwenda kujadili uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya kutupa shauri lao, walikubaliana kukata rufaa kwa lengo la kutafuta haki mahakama za juu.

“Baada ya kukubaliana kuendelea na kesi yetu mahakama ya juu, suala hili kimahakama tumemuachia mwanasheria wetu ambaye analishughulikia, lakini ameshatuambia tayari rufaa yetu imeshapokelewa Mahakama Kuu hivyo tunachosubiri ni kutupangia tarehe ya kwenda kusikiliza,”alisema.

Alisema tayari ndugu walishatawanyika msibani kwa ajili ya kwenda kuendelea na shughuli nyingine na wakihitajika mahakamani wataitana na kupeana taarifa.

“Sisi hatujagoma kumzika kijana wetu, lakini tunachohitaji ni kuona unafanyika uchunguzi wa kidaktari ili kubainisha sababu hasa ya kifo chake, maana tunaona kuna kama ujanjaujanja unataka kufanyika.”

Jalada latua Mahakama Kuu

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, George Herbert wiki mbili zilizopita aliliambia Mwananchi kuwa tayari jalada la hukumu ya kesi hiyo limeshafika kwa Jaji Mfawidhi na kinachosubiriwa ni kupangiwa jaji atakayebeba jukumu la kusikiliza rufaa hiyo.

“Tulikuwa tunasubiri jalada la hukumu kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya na sasa limeshafika, hivyo Jaji Mfawidhi atampanga jaji wa kusikiliza na ndugu wataarifiwa ndani ya muda mfupi,” alisema Herbert.

Uongozi wa Hospitali ya Rufaa.

Awali, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi kutupa maombi ya familia hiyo, pia ilitoa amri kwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kuutoa mwili kwa ndugu ama kuuzika.

Hata hivyo, ulishindwa kutekeleza amri hiyo kutokana na kupokea hati ya rufaa kutaka kutotelekezwa kwa amri hiyo kwa vile kesi hiyo imepelekwa Mahakama Kuu.

Katika maelezo ya mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mteite, Septemba 2 ilitoa amri kwa mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk Godlove Mbwanji kuutoa mwili huo na kuwakabidhi ndugu wakauzike kama zilivyo tamaduni za Kiafrika badala ya kuendelea kuuacha mochwari.

Pia, mahakama hiyo ilielekeza endapo ndugu hao watagoma kwenda kuuchukua mwili huo, uongozi wa hospitali kwa kushirikiana na kitengo cha afya cha Jiji la Mbeya wafanye taratibu za kwenda kuuzika.

Dk Mbwanji alisema kabla ya kutekeleza amri hiyo, alipelekewa hati ya rufaa kutoka kwa wakili wa familia ya Kapange inayoonyesha kwamba wamekataa rufaa juu ya amri hiyo.

Kutokana na hati hiyo waliamua kusitisha mchakato wa kutekeleza amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Mbeya hadi utakapotolewa uamuzi mwingine kulingana na rufaa waliyokata ndugu hao.