Matukio ya utekaji wa watoto yawaibua polisi

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi nchini limetaja mambo kadhaa ambayo wazazi wanatakiwa kuyafanya ili kuhakikisha watoto wao wanakuwa katika mikono salama huku akisisitiza kuwa hilo halizuii wajibu wa polisi wa kuzuia makosa

Dar es Salaam. Wakati matukio ya utekaji watoto yakizua mjadala kila kona nchini, Jeshi la Polisi limesema baadhi ya matukio hayo yanatokana na uzembe wa wazazi.

Akizungumza leo Jumanne Oktoba 2, 2018 msemaji wa jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwaamesema polisi ni wataalamu wa kuzuia makosa na wazazi wana jukumu la kuhakikisha watoto wao wanapokuwa mahali popote wanakuwa na ulinzi ili wasiingie katika mikono ya wahalifu.

Amewataka wazazi wanapowaacha watoto nyumbani wawafundishe kutokubali jambo lolote watakaloelezwa na mgeni wasiyemfahamu.

 “Kwa mfano kuna mtu anacheza na mtoto wako humjui au unamfahamu juu juu tu na upo eneo hilo lakini unatazama tu.  Siku huyo mtu akija na kutaka kuondoka na mtoto wako sidhani kama anaweza kukataa,” amesema.

Mwakalukwa ametaja jambo lingine ni wazazi kuwa makini na wasaidizi wa kazi za majumbani ambao muda mwingi hubaki na watoto, kushauri walipwe vizuri.

“Una migogoro na dada wa kazi kila siku, anakudai hutaki kumlipa unadhani atafanya nini kujitetea, haijulikani atachukua hatua gani,  anaweza kuondoka na mtoto nani anajua?” amehoji.

Amesema wazazi wasiishie hapo badala yake wawe karibu na walimu ambao hukaa muda mwingi na watoto wao shuleni.

“Pia wawe na namba za madereva wa magari ya shule ili ikitokea jambo lolote waweze kufuatilia kwa ukaribu,” amesema Mwakalukwa.

Amefafanua kuwa kwenye nyumba za ibada ielezwe umuhimu wa familia zenye watoto kuhakikisha kuwa wanapokuwa eneo hilo watoto wanakuwa salama.

Amewataja wengine wanaopaswa kujumuika na wazazi kulitokomeza hilo kuwa ni viongozi wa dini na wanaharakati wa masuala ya watoto.

“Mambo mengi yanasababisha watoto kupotea ikiwamo wanaotaka kwenda kuwalawiti kwa tamaa za kimwili, wanaowatorosha kwa nia ya kulipa visasi, wakati mwingine ni utapeli, hivyo  wazazi wasiache taarifa za namba zao za simu kwa watu wasiowafahamu,”amesema.