Sintofahamu madai ya kukamatwa kwa Nondo

Muktasari:

Profesa Mfinanga alitoa ufafanuzi huo jana baada ya Nondo kudaiwa kukamatwa na polisi akiwa maeneo ya chuo hicho, huku wakili wa mwanafunzi huyo, Jebra Kambole akisema alikamatwa juzi.

Dar es Salaam. Saa chache baada ya kusambaa kwa taarifa za kukamatwa kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSN), Abdul Nondo, naibu makamu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Davidi Mfinanga amesema hana uhakika kama Nondo alizuiwa kuonekana maeneo ya chuo hicho.

Profesa Mfinanga alitoa ufafanuzi huo jana baada ya Nondo kudaiwa kukamatwa na polisi akiwa maeneo ya chuo hicho, huku wakili wa mwanafunzi huyo, Jebra Kambole akisema alikamatwa juzi.

Hata hivyo, gazeti hili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kuzungumzia madai hayo alisema yupo kikaoni.

Machi 26 mwaka huu, Nondo alisimamishwa kuendelea na masomo UDSM baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa.

Nondo anatuhumiwa kwa makosa mawili likiwamo la kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni Machi 7, mwaka huu akiwa Ubungo na kusambaza kwa kutumia mtandao wa WhatsApp kuwa yupo hatarini.

Shtaka lingine ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma alipokuwa akitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mafinga kuwa alitekwa na watu wasiojulikana Dar es Salaam na kupelekwa Kiwanda cha Pareto cha Mafinga.

Akizungumza na Mwananchi wakili Kambole alisema Nondo alikamatwa juzi saa tatu usiku kwa kile kinachodaiwa kuingia eneo la chuo hicho kinyume na sheria.

Alisema katika barua ya kumsimamisha masomo Nondo, haikueleza kuwa hatakiwi kuonekana eneo la chuo hicho.

Kambole alisema lengo la Nondo kufika chuoni hapo ilikuwa ni kuchukua vitabu alivyoviacha baada ya kupewa barua ya kusimamishwa masomo.

“Lakini eneo alilokamatwa mtu yeyote anaweza kupita kwa sababu hata magari ya kwenda Mwenge yanapita,” alisema Kambole.

Akizungumzia suala hilo, Profesa Mfinanga aliomba kupewa muda zaidi ili aweze kufuatilia.